Wajadili ubunifu sekta ya utalii

KATIKA kuadhimisha siku ya Mwanamke Duniani, Wanawake wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na taasisi ya The Fungua Trust  kwa pamoja wamejadili namna gani wanawamke wanashiriki kuwa wabunifu katika masuala mazima ya  teknolojia hasa sekta ya utalii.

Katika mjadala huo ambao uliongozwa na mgeni rasmi mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango na Maendeleo  (UNDP) Christine Musisi ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi saba za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi wa The Fungua Trust na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki anayewakilisha Tanzania Shogo Mlozi akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, alisema  mijadala hiyo inalenga kutoa elimu ya moja kwa moja katika masuala ya utalii na masuala mengine mtambuka.

Advertisement

Alisema kama wanawake wanataka kuona masuala mbalimbali ambayo yanamlenga mwanamke ili kuweza kuhakikisha wanatoa michango mbalimbali itakayoenda kubadilisha katika sera mbalimbali zinazoweza kuwa sera za Tanzania au sera za nchi za Afrika Mashariki.

“Mjadala huu utakuwa wa muhimu sana lakini pia tunafurahi, kwakuwa sisi wabunge wanawake wa Afrika Mashariki masuala haya tunayoyajadili, yataweza kuleta tija katika kuleta uelewa wa pamoja pia kuhakikisha yanapelekea kubadilisha sera mbalimbali zitakazo mwezesha mwanamke kuwa na mchango mbalimbali katika maeneo ya uongozi au maeneo mengine” alisema.

Aliongeza kwa kusema mijadala mingine itajikita katika Uongozi kwa wanawake hasa katika Utalii, kukua kwa teknolojia katika sekta ya utalii, utalii wa Afya na Tiba, teknolojia katika masuala ya kilimo, elimu ya utalii na mabadiliko ya tabia nchi inavyoathiri sekta ya utalii.

Aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za Uwaziri na kuwa waziri aliyekaa kwa muda mrefu katika wizara ya Maliasili na  Utalii kwa miaka tisa na waziri wa kwanza mwanamke  Wizara ya Fedha Zakia Meghji alisema masuala ya  teknolojia yamesaidia sana kuwapa nafasi wanawake.

Alisema wakati wake ilikuwa ngumu sana kukuta wanawake wakifanya kazi kama ya kuendesha ndege, kuendesha magari makubwa au kuendesha matrekta kitu ambacho kwasasa kinafanyika.

“Kipindi chetu hata katika elimu unaweza kwenda shule na kukuta wasichana wachache au hata mkawa sawa, lakini kadri mnavyozidi kupanda juu unakuta wanawake wanapongua tofauti na sasa” alisema Meghji.

Latina majadiliano hayo pia walishiriki wabunge kutoka nchi saba za Afrika Mashariki na viongozi wengine kutoka katika Serikali za nchi hizo.