Wajasiriamali kupewa elimu uzalishaji bidhaa bora

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amewaagiza wataalam wa uthibitisho wa ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), TMDA na SIDO kuwaelimisha wajasiriamali namna ya kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Akizungumza katika uzinduzi wa maonesho ya biashara ya Tanzanite wilayani Zindagi mkoani Manyara leo Oktoba 18, Kigahe ameutaka Mkoa wa Manyara na halmashauri zake kuendelea kushirikiana na waratibu wa Bodi ya Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) kusogeza huduma karibu ili wajasiriamali washiriki maonesho.

Amesema baadhi ya wajasiliamali hawana elimu ya kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika solo la kimataifa hivyo kuzalisha bidhaa zisizothibitishwa na mamlaka husika kama zimekidhi ubora.

Advertisement

Taasisi za serikali na binafsi  zikiboresha mazingira ya uwekezaji zitatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza na kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa kuwa wataweza kuzalisha bidhaa zitakazopata soko katika masoko ya Dunia,” Amesema Kigahe.

“Kupitia maonyesho haya wafanyabiashara wadogo na kati wachimbaji wa madini, wakulima, wasindikaji wa mazao ya ndani wataweza kuunganishwa katika upatikanaji wa masoko, mashirika ya udhibiti na upatikanaji wa matangazo ya biashara”.ameongeza.

Kagahe Amebainisha kuwa uhamasishaji wa umma juu ya bidhaa zinazozalishwa nchini, madini na viwanda mbalimbali utaongezeka.

“Mahusiano haya yatasaidia kumaliza changamoto za wafanyabiashara na kumsaidia kuongeza idadi ya washiriki wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya madini ya Tanzanite na kilimo”. Amesisitiza Kigahe.

Aidha ameutaka mkoa huo kutenga eneo maalum kwa ajili ya maonesho ili kuboresha na kuwa na miundombinu ya kisasa.

Meneja masoko wa Kampuni ya Mati Super Brand Ltd Elvis Peter amesema maonesho hayo yanaunga mkono nia ya serikali ya kuharakisha maendeleo katika kuwasaidia wajasiliamali na wawekezaji kukidhi mahitaji ya jamii.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Manyara, Musa Msuya ameishukuru serikali kwa kukubali kujenga kiwanja cha ndege katika mkoa huo kwakuwa utaongeza idadi ya wawekezaji na watalii.

5 comments

Comments are closed.