WAJASIRIAMALI wametakiwa kutambua umuhimu wa bima na kuwa na bima za biashara, ili wanapopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo moto, kuharibikiwa mali na ugonjwa waweze kufidiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bima ya Fortis, Maryam Shamo amebainisha hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari, wakati wa uzinduzi wa Malkia Bima uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Fortis kwa kushirikiana na taasisi ya bima ya Assemblies, walizindua huduma ya hiyo ya Malkia akaunti, kwa lengo la kumnufaisha mjasiriamali mwanamke kufikia malengo yake akiwa na ulinzi wa bima hiyo.
Maryam alisema wameamua kuanzisha akaunti hiyo ya bima kwa lengo la kuwanufaisha wanawake mmoja mmoja au kwenye vikundi.
“Akaunti hii itasaidia wanawake walioko kwenye vikundi kama vile ikoba, saccos ,vikundi vya akina mama na wafanyabiashara wanapopata maafa yanayosababishwa na moto na viashiria vya hatari zake, kukatizwa kwa biashara kunakotokana na moto au kuvamiwa na majambazi,” alisema Maryam.
Alisema Malkia Bima ina faida kubwa ikiwa ni pamoja na ushauri wa afya baada ya maafa ya moto, ajali binafsi, kulipiwa fedha hospitali pindi mtu anapopatwa na maradhi na huduma nyinginezo.
Alieleza kuwa bima hiyo ni rahisi kufungua na inagharimu kiasi cha Sh 8,000 tu.
Naye Mkurugenzi wa taasisi ya Bima ya Assemblies, Tabia Massudi alisema wameamua kuungana pamoja, ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuhamasisha kila Mtanzania awe na bima.
Hata hivyo, alisema licha ya kwamba bima inajulikana kama Malkia, lakini kila mjasiriamali atanufaika nayo bila kujali jinsi yake.