Kukimbia ni mchezo rahisi ni sanaa ya kuweka mguu mmoja mbele ya mwingine kwa kasi zaidi kuliko washindani wengine iliyotumiwa na washindi wa mbio za hifadhini za Great Ruaha Marathon.
Mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zikiwa na ujumbe mzito wa kulinda vyanzo vya maji na kutangaza utalii wa ndani zilihusisha wakimbiaji zaidi ya 350 wakiwemo washiriki kutoka bara la Ulaya na Asia.
Wakimbiaji kutoka bara la Ulaya waling’ara zaidi katika mbio za kilometa tano, 10 na 21 za wanawake na wanaume huku watanzania wakitanua bila upinzani katika mbio za kilometa 42.
Katika mbio za kilometa tano wanawake, mjerumani Regina Runmers alitumia dakika 32 kushinda mbio za kilometa tano huku Nicola Schliter akitumia dakika 59 kushinda za kilometa 10 na Julia May akitumia saa 1:49 kuwa mshindi wa pili wa kilometa 21.
Wazungu wengine walioingia nafasi tano za juu na kuahidi kuanza mapema maandalizi ya kushiriki mbio zitakazofanyika tena mwakani ni pamoja na Yohannes Boneff, Warren Zambetakis, Emmanuel Manas, Faye Osborn, Emanuel Eser, Bruce Arndtt na Ucly Heichogan aliyekuwa mshindi wa tatu wa mbio za kilometa 10 wanawake.
Kwa upande wa mbio za kilometa 42 wanawake watanzania walioshinda walikuwa Mbisa Luhalwa aliyetumia saa 3:21 na Shamia John aliyetumia saa 3:50 huku nafasi ya kwanza kwa wanaume ikienda kwa Tumaini Habie aliyetumia saa 3:07, wa pili Leonard Ilapsha saa 3:42 na ya tatu ilienda kwa mzee wa zaidi ya miaka 60, Yona Mwalusamba aliyetumia saa 3:59 kuwagaragaza vijana.
Watazania wengine waliopachomoza katika nafasi tatu za juu za mbio za kati ya kilometa tano na 21 ni pamoja na Greyson Mahimbi, Hoza Mbuya, Winnifrida Njilima, Magreth Daudi, Arifu Juma, Beni Kashiririka na Manfred Kimano, Atuganile Mfikwa, Catherine Simfukwe na Pascal Bilingi, Cresto Muhonja, Issack Kivamba na Samwel Nyangula.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi , Godwell Ole Meing’ataki alisema wakati washindi hao wakikabidhiwa medali na zawadi zao (vikiwemo vyeti na fedha taslimu) kwamba Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) litatoa ofa kwa washindi wote wa kwanza wa mbio hizo kutalii kwa siku mbili katika hifadhi hiyo kwa gharama zao.
Akikabidhi zawadi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy alisema; “Wengi tulikuwa hatuamini kama tunaweza kukimbia sehemu yenye wanyama wakali, lakini hilo limewezekana na tumeunga mkono juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan za kutangaza na kukuza utalii wetu.”
Aliwaomba washiriki wa mbio hizo wakawe mabalozi wa ulinzi wa vyanzo vya maji yanayotiririka kuelekea mto Ruaha Mkuu ambao ni tegemeo la maji kwa wanyama wa hifadhi ili visihaharibiwe na shughuli za binadamu kwasababu maji yake ni muhimu kwa shughuli za uhifadhi, utalii, kilimo, uvuvi, matumizi ya majumbani na viwandani na uzalishaji wa umeme.
Mbio hizo za Great Ruaha Marathon zilizoratibiwa na Shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zilidhaminiwa na Mabata Makali Lodge and Campsite, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kampuni ya Asas Groups Ltd.