MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa amewataka maofisa ugani wa mkoa wa Morogoro kuwajibika kwa wakulima katika kutoa elimu ya kilimo bora, kitakachowawezesha kuongeza tija ya uzalishaji baada ya kupatiwa nyenzo ya usafiri wa pikipiki na serikali.
Nsemwa amesema hayo Machi 27, 2023 kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki 436 kwa maofisa ugani wa mkoani Morogoro akimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa.
Amesema kutokana na kuwezeshwa usafiri wa pikipiki hivi sasa, wanao uwezo kuwafikia wakulima wengi zaidi hata wale waliopo maeneo yenye changamoto ya usafiri.
Amesema kwa sasa anatarajia uzalishaji kwenye sekta ya kilimo utaongezeka, kwa sababu wataweza kuwafikia wakulima kwa wakati na kutekeleza majukumu yao kwa wakati unaotakiwa.

“Tuna uhakika uzalishaji wetu maeneo yetu ya kilimo kwa sasa utakwenda kuimarika kwa sababu wataalamu wetu watakwenda kuwafikia au kumfikia mkulima mmoja mmoja na kumpatia elimu ya kilimo bora chenye kuleta tija, ” amesema Nsemwa.
Mkuu wa wilaya hiyo amesema pikipiki hizo zigawiwa kwa maofisa hao wa kila kata kwenye kila halmashauri za mkoa wa Morogoro.
Naye Katibu Tawala Msaidizi upande wa Uchumi na Uzalishaji , Dk Rozalia Rwegasira katika taarifa fupi kuhusiana na pikipiki hizo amesema zimefungwa kifaa maalumu, ambacho kinaonesha mahali ambapo pikipiki hiyo ipo kwa wakati huo.
Amesema pikipiki hizo zitawasaidia maofisa ugani kupata takwimu sahihi za wakulima katika maeneo yao, pamoja na kuwahudumia bila shida yoyote.