Wajipanga kutoa elimu mchakato Katiba mpya

TAASISI ya Foundation for Civil Society (FCS), imesaini mkataba wa Sh bilioni nne na taasisi nyingine tatu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mchakato wa katiba mpya, ambao unakaribia kuanza baada ya Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kumuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga kabla ya utiaji saini huo amesema hilo limefanyika kwa kuwa lengo lao kuu ni kuongeza hamasa, ushiriki na wigo wa ushiriki wa wananchi katika utawala bora kuhusiana na mchakato huo wa katiba mpya, ambao ulianza lakini haukufika mwisho.

Ametaja taasisi nyingine iliyosaini nazo mkataba huo kuwa ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) Pamoja na Jumuiya ya Mashirika yasyo ya kiserikali (Tango).

Kwa maelezo ya Kiwanga kazi kubwa ya FCS ni kuwezesha asasi za kiraia kuimarisha utawala bora nchini pamoja kuongeza uwezo wa Watanzania wote kujikimu.

“Leo tumefanya uzinduzi wa mpango kabambe wa miaka mitatu unaoitwa uraia wetu. Jukumu kubwa lilipo mbele yetu kama taifa, sasa hivi serikali imepiga filimbi ya kuashiria mwanzo wa mchakato wa maandalizi ya katiba mpya na hivyo basi sisi tukishirikiana na wadau wengine wa maendeleo tumeamua kuja na mpango huo wa miaka mitatu wenye lengo kubwa la kufanya kila mwananchi kwa kadri anavyoweza kushiriki katika mchakato huo,” amesema.

Amesema wamesaini mkataba huo na TLS kwa sababu ni wataalam wa sheria, hivyo watasaidia kuongoza na kufanya kazi na wananchi katika kazi nzima ya kutengeneza katiba.

Vilevile amesema Jukata kama jukwaa la wananchi wanaamini, litafika katika mikoa na wilaya zote nchini kutoa elimu, ili sauti za wananchi ziweze kuingia katika mchakato huo.

Amesema Tango ni mdau mkubwa kwa kuwa ni mwavuli wa asasi zote za kiraia, ambazo nazo zinashiriki katika mchakato huo.

Naye Mwakilishi kutoka TLS, Maekphason Mshana, amesema wamejipanga vizuri katika program hiyo kwa kuwa shughuli yao kubwa ni kuangalia sheria zote zinazohusiana na sheria ya mchakato wa uchaguzi kwa kuwa kuanzia mwaka kesho kutakuwa na chaguzi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo kwa asasi za kiraia, ili ziwe na uhusiano mzuri na serikali pamoja na wadau mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata, Bob Wangwe amesema wataangalia eneo la katiba namna gani wanashirikisha asasi katika mchakato huo pamoja na wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tango, Adamson Nsimba amesema watahakikisha asasi za kiraia zinakuwa mstari wa mbele ili kuwa na uhusiano mzuri na serikali, lakini kuhakikisha sauti za watu zinasikika.

Habari Zifananazo

Back to top button