WAKALA wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA) imejipanga ifikapo mwaka 2030 kuzalisha tani 30,000 za chai kavu iliyosindikwa ili kuwainua kiuchumi wakulima wadogo wa zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TSHTDA, Theophord Ndunguru wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mikakati iliyowekwa kwenye uzalishaji wa zao hilo ili mkulima mdogo wa chai nchini aweze kupiga hatua kwenye kilimo hicho.
Alisema kwa sasa wakulima hao wanazalisha tani 13,000 ambazo hazijitoshelezi, hivyo moja ya mkakati waliyojiwekea kama wakala ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka.
“Miongoni mwa mikakati yetu ni kujipanga kuhakikisha wakulima wanafikia uzalishaji tani 30,000 za chai kavu iliyosindikwa, naamini itafikia hivyo kutokana na serikali kutoa mbolea ya ruzuku,” alisema. Pia alisema wamejipanga kufanya utafiti wa soko la bei ya chai duniani ili kutatua changamoto ya wakulima wadogo wa zao hilo hapa nchini.
Ndunguru alisema moja ya changamoto inayowakabili wakulima ni uuzaji wa chai kwa bei ndogo, jambo linalosababisha kushindwa kumudu kulima kwa wingi zao hilo.
Akizungumzia utoaji huduma, alisema TSHTDA wameingia mkataba na kampuni kadhaa kwa ajili ya kutoa huduma za ugani wakati wowote kwa wakulima katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo aliwataka wakulima kuchangamkia fursa ya mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali ili kuhakikisha wanalima kwa wingi zao hilo.
Ndunguru alisema awali wakulima wengi wadogo walishindwa kumudu kununua mbolea kutokana na bei kubwa lakini hivi sasa changamoto ya mbolea inakwenda kumalizika kutokana na serikali kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima.