Wajumbe wameamua

DAR ES SALAAM; WAJUMBE wa mikutano mikuu ya kata, wadi na jimbo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepiga kura za maoni kuchagua wagombea wa ubunge, udiwani Tanzania Bara, ujumbe wa baraza la wawakilishi na wadi kwa Zanzibar.

Aliyekuwa Mbunge wa Bukombe katika Bunge la 12, Dk Doto Biteko amepata kura za ndiyo 7,441 kati ya kura halali 7,441.

Wajumbe 7,456 walihudhuria uchaguzi huo zikapigwa kura 7,456, kura 15 ziliharibika.

Dk Biteko alikuwa mgombea pekee wa ubunge kupitia CCM katika jimbo hilo.

Tanga

Aliyekuwa mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdulrahaman Shillow ameshindwa kwenye kura za maoni kwenye Kata ya Mzingani baada ya kupata kura 68 kati ya 334.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Balqis Abdallah alisema zilipigwa kura 333 na mgombea Hamza Bwanga alipata kura 263 na kura tatu ziliharibika. Bwanga ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Tanga.

 Dodoma

Aliyekuwa Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye sasa anagombea katika Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde alikuwa anaongoza katika kata sita kati ya 20 za jimbo hilo.

Katika Kata ya Makole, Mavunde alipata kura 107, Mussa Luhamo kura tano na Anthony Kanyama kura sita katika ya kura 120 zilizopigwa.

Kwenye kata ya Kiwanja cha Ndege, Mavunde alipata kura 124, Kanyama 12, Mwajuma Karabaki nne, Luhamo tatu kati ya kura 145 zilizopigwa.

Kata Msalato Mavunde alipata kura 153, Kanyama sita, Mwajuma tano, Luhamo 25 kati ya 188.

Kata ya Mtumba alipata Mavunde 189, Kanyama 24, Mwajuma nne, Luhamo 54 kati ya 273.

Katika kata ya Iyumbu alipata Mavunde alipata 138, Kanyama saba, Mwajuma moja, Luhamo saba na katika Kata ya Ipagala Mavunde alipata kura 192, Luhamo 13, Kanyama 12 na Mwajuma mbili.

 Arusha

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameongoza kura za maoni za ubunge wa Arusha Mjini kwa kupata kura 9,056 kati ya kura halali 9,265 sawa na asilimia 97.63 ya kura zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ofisi za CCM Wilaya ya Arusha zilipigwa 9,276, kura halali zilikuwa 9,265 na kura 11 ziliharibika.

Mustapha Nassoro alipata kura 83 (0.89%), Hussein Gonga kura 46 (0.50%), Ally Babu kura 28 (0.30%), Aminata Traore kura 26 (0.28%), Ruwembo Nkwavi kura 16 (0.17%) na Jasper Kishumbua kura 10 sawa na asilimia 0.11.

Kata ya Ngarenaro mgombea Abdulazizi Abubakar maarufu kwa jina la Dogo Janja ameongoza kwa kupata kura 76, Diwani aliyemaliza muda wake, Isaya Doita alipata kura 60 na Benjamin Mboyo kura mbili.

Katika kata ya Themi, Melance Kinabo ameongoza kwa kupata kura 115, nafasi ya pili ilishikwa na aliyekuwa diwani wa kata hiyo Lobora Ndarpoi na nafasi ya tatu ilishikwa na Catherine Nyabamba aliyepata kura 12.

Katika kata ya Moshono, Siriel Mbise aliongoza kwa kupata kura 112, nafasi ya pili ilishikwa na Miriamu Kisawike aliyekuwa diwani katika kata hiyo aliyepata kura 80 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Emmanuel Munga.

 Moshi

Mbunge Moshi Mjini aliyemaliza muda wake, Priscus Tarimo ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 1,539 akimshinda mpinzani wake wa karibu, Ibrahim Shayo aliyepata kura 1,495.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Ivan Moshi alitaja wagombea wengine ni Amin Twaha aliyepata kura 143, Samuel Ngowi (67), Theresia Komba (36) na Profesa Neema Kumburu aliyepata kura nane.

Moshi alisema zilipigwa kura 3,298, kura halali zilikuwa 3,288 na kura 10 ziliharibika.

Pangani

Katika Jimbo la Pangani mkoani Tanga, Jumaa Aweso ameongoza katika kura za maoni baada ya kupata kura zote za ndiyo katika kata zote kwenye jimbo hilo.

Mbeya

Diwani wa Kata ya Sisimba jijini Mbeya aliyemaliza muda wake, Josephine Kamonga aliongoza kwa kupata kura 127.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Yusuph Gilison alisema Josephine alifuatiwa na Martini Mutayoba aliyepata kura 13, Moses Mwidete kura tisa na Geofrey Kajigiri kura mbili.

Gilison alisema katika uchaguzi huo kulikuwa na wagombea wanne na wajumbe 183 walihudhuria.

Kwa upande wa kura za maoni kwa nafasi ya ubunge katika kata hiyo, Patrick Mwalunenge ameongoza kwa kupata kura 98 akifuatiwa Dk Mabula Mahande kura 24, Sambwee Shitambala kura 14, Charles Mwakipesile kura nne, Elizabeth Maginga kura moja na Sophia Malingumu aliyepata pia kura moja.

 Dar es Salaam

Kibamba

Katika Jimbo la Kibamba hadi tunakwenda mitamboni Angela Kairuki alikuwa anaongoza kwenye kata nne kati ya sita.

Kinondoni

Hadi tunakwenda mitamboni taarifa zilidai Abbas Tarimba alikuwa anaongoza kura za maoni jimbo la Kinondoni.

Manara kidedea

Kada wa CCM Haji Manara ameongoza kura za maoni za kuwania nafasi ya udiwani katika Kata ya Kariakoo mkoani Dar es salaam akiwashinda wagombea wenzake wanne.

Manara amepata kura 136, Daudi Simba kura 85, diwani aliyemaliza muda wake, Abdul Masamaki kapata kura 31 na Siza Mazongela hakupata kura hata moja.

Shetta ang’ara

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nurdin Bilal Juma maarufu ‘Shetta’ ameongoza kura za maoni nafasi ya udiwani Kata ya Mchikichini wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam.

Shetta aliwazidi wapinzani wake kwa kupata kura 293, Azimkhan Akber Azmkhan amepata kura 178 na Joseph Ngowa kura saba.

Josephine Wage ameongoza kura za maoni Kata ya Hananasif kwa kupata 145, Said Mfaume amepata 125. 

Mbinga Vijijini

Kura za maoni ubunge Jimbo la Mbinga Vijijini, Judith Kapinga ameongoza kura katika kata 13 kati ya 15 na Mbunge aliyemaliza muda wake, Benaya Kapinga ameongoza kata mbili.

Makambako

Hadi tunakwenda mitamboni mgombea Daniel Chongolo alikuwa anaongoza katika kata 10 kati ya 12 za jimbo hilo.

Katika kata ya Kivavi amepata 985, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Deo Sanga amepata kura 35.

Kata ya Majengo Chongolo kapata kura 289, Sanga 13, Kata ya Kitisi Chongolo kura 376 na Sanga kura 68.

Kwenye kata ya Utengule, Chongoo kapata kura 605, Sanga kura 45, Kata ya Makakambo Chongolo kapata kura 574 na Sanga kura 26.

Katika Kata ya Mwembetogwa, Chongolo amepata kura 175, Sanga kura 16, Kata ya Mjimwema, Chongolo amepata kura 318 na Sanga kura 26.

Kwenye Kata ya Laymkena, Chongolo amepata kura 319, Sanga kura 19, Kata ya Mahongole, Chongolo kapata kura 761, Sanga kura 74 katika Kata ya Mlowa Chongolo kata kura 731 na Sanga kura 13.

Bukoba Mjini

 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bukoba Mjini, Shabani Mdohe ametangaza Johnston Mtasingwa ameongoza kura za maoni kwa kura 1,408.

Mdohe alisema wagombea wengine Alex Denis alipata kura 804, Almasoud Kalumuna kura 640 Jamila Hassan kura 66 na Koku Rutha kura 44.

Alisema wapigakura waliojiandikisha ni 3,033 waliojitokeza kupiga kura ni 2,978 na kura 20 ziliharibika na kura halali ni 2,958.

Nyasa

Katika Jimbo la Nyasa aliyekuwa Mkurugenzi wa Miji la Mbeya, John Nchimbi anaongoza kwenye kura za awali akiwashinda wagombea wengine watano.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo kesho kamati ya siasa ya jimbo itawajadili wagombea ubunge, udiwani Tanzania Bara na uwakilishi na wadi kwa upande wa Zanzibar na kutoa mapendekezo kwa kamati ya siasa ya wilaya.

Vikao vya Kamati za siasa za wilaya vitafanyika Agosti 8 kujadili wagombea ubunge, ujumbe wa baraza la wawakilishi na udiwani na kutoa mapendekezo kwa kamati ya siasa ya mkoa.

Imeandikwa na Ikunda Erick (Dar es Salaam), John Mhala (Arusha), John Nditi (Morogoro), Shukuru Mgoba (Mbeya), Amina Omari (Tanga), Anastazia Anyimike (Dodoma) na Diana Deus (Bukoba).

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button