Wakamatwa kwa kuendesha kiwanda bubu cha pombe
POLISI mkoani Morogoro inawashilia watu wanne kwa tuhuma za kuendesha kiwanda Bubu cha kutengeneza na kusambaza bidhaa bandia ya pombe kali aina ya Smart Gin katika mtaa wa Tushikamane kata ya Lukobe ,Manispaa ya Morogoro.
Watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na chupa zilizojazwa 2,544 aina ya pombe hiyo, chupa tupu 2,988 ,chupa za Konyaji zilizojazwa 65, chupa tupu mbalimbali za konyaji zikiwa ndani ya mifuko minne ya salfeti, boxi moja, madumu lita 20 yaliyojazwa spiriti na mengine yenye mchanganyiko wa spiriti na maji .
Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Alex Mkama amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kufanyika kwa oparesheni na misako mbalimbali mwishoni wa Desemba mwaka huu.
Mkama amesema katika opereshani hiyo, polisi walifanikiwa kuwakamata Ramadhani Mdoe ( 30) mkazi wa Msamvu, Manispaa ya Morogoro na wenzake watatu kwa tuhuma za kukutwa wakitengeneza na kusambaza bidhaa feki ya pombe kali aina ya Smart Gin.
Ametaja baadhi ya vitu vingine walivyokutwa navyo ni jaba tatu kwa ajili ya kuchanganya na kuchuja pombe, gundi chupa tano, stika 2,037 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lebo 6,226 za Smart Gin, na lebo za konyagi kubwa na ndogo 10,886.
“Shughuli zote hizi zilikuwa zinafanyika kwenye kiwanda bubu kilichopo katika mtaa wa Tushikakame, kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro na watuhumiwa wanashirikiwa na kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi na watafikishwa mahakamani “ amesema Mkama.
Katika hatua nyingine, polisi wanamshikilia Richard Paul (39) mkazi wa Kihonda na wenzake wawili kwa tuhuma za kufanya shughuli za uganga bila kibali kwa kupiga ramli chonganishi jambo ambalo limesababissha kutokea kwa migogoro katika jamii na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa kuwa, watuhumiwa hao wanahojiwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.