Wakandarasi waliofanya vizuri watunukiwa

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya ukandarasi ya Steg International Services, imekuwa mshindi wa kwanza katika tuzo za mwaka 2024 zilizotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kumaliza miradi inayopewa kabla ya muda uliopangwa.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy ameeleza hayo baada ya kukabidhi tuzo kwa wakandarasi 19 waliofanya vizuri katika miradi yao.

Saidy akielezea kampuni hiyo amesema, mara zote mshindi huyo wa jumla amekuwa akimaliza miezi miwili ama mitatu kabla ya muda waliopewa.

” Ukimpa miezi 18, miezi 15 anakupa kazi miezi mitatu kabla. Kazi ya mwisho alikuwa amalize Septemba mwaka jana lakini alimaliza Juni,” amesema.

Meneja Mradi kampuni hiyo, Shaban Zacharia amesema wamepata ushindi huo ni mipango mizuri ya kazi na kujituma kutekeleza mipango hiyo.

Washindi wengine kati ya watano bora waliopata tuzo hiyo ni Ms China Railway Construction, Ms Sengerema Engineering, Wooden Plaque na Sagmcom.

Amewataka wakandarasi kukamilisha miradi mbalimbali wanayotakiwa kuitekeleza kwa maelezo kuwa REA wapo tayari kufanya kazi na kuwapa miradi mbalimbali wale wanaoikamilisha kwa wakati.

“Utendaji wa wakandarasi hao utawapa nafasi ya kufanya kazi nyingi za REA na nyinginezo,”amesema.

Amesisitiza ikifika Julai mosi mwaka huu watakaoomba kazi zitakazotangazwa na wakala huo wawe ni wale waliomaliza kazi zao kwa wakati.

Katika hilo alionya tabia ya wakandarasi kuacha tabia ya kuchonganisha wananchi na serikali katika miradi wanayopewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) , kwa kuongeza maeneo wanayopangiwa kufanya kazi.

“Hatutaki kwa namna yoyote miradi yetu ichonganishe wananchi na serikali. Zipo kesi wakandarasi wanaambiwa kupima kilomita mbili, lakini anatuletea kilomita tatu.

“Hata kama ni matamanio kupeleka umeme maeneo yote, kuna suala la uwezo. Hili linaleta rushwa ama tuhuma za rushwa,”amesema.

Awali Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu amesema mpaka sasa jumla ya vijiji 11,839 kati ya 12,318 vimepatiwa umeme.

Pia amesema pamoja na mafanikio hayo, uhitaji wa umeme kwa wananchi ni mkubwa kuliko uwezo wa kifedha.

 

Habari Zifananazo

Back to top button