WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itamkumbuka aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Hassan Wakasuvi kutokana na mchango wake mkubwa katika shughuli za maendeleo nchini.
Amesema hayo leo (Jumamosi Februari 24, 2024) alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maziko ya Wakasuvi yaliyofanyika katika kijiji cha Mabama mkoani Tabora.
Amesema kuwa Wakasuvi alikuwa kiongozi imara katika kusimamia shughuli za maendeleo ikiwemo sekta ushirika nchini na umahiri wake uliwezesha kuimarika kwa sekta hiyo na kuleta tija nchini.
“Aliiwakilisha nchi vyema kwenye sekta ya ushirika sio Tanzania tu, bali Afrika Mashariki, Ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Afrika kwa ujumla. ”
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk Emmanueli Nchimbi amesema Wakasuvi alikuwa na kiwango kikubwa cha kuaminika.
Ameongeza kuwa Wakasuvi alikuwa kinara katika kuchochea umoja ndani ya CCM pamoja na maendeleo ndani ya nchi. Leo “Chama, Serikali na Wananchi tumepoteza kiongozi mahiri, tumuenzi kwa kuendeleza umoja na mshikamano.”