Wakazi Arusha Chini waanza kusahau kero ya mafuriko

WAKAZI waishio ukanda wa tambarare hususani katika Kata ya Arusha Chini iliyopo Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakikumbwa na adha ya mafuriko ya mara kwa mara hali inayosababisha wakazi hao kuishi maisha ya hofu, kuombaomba na taharuki.

Mafuriko hayo kwa kiwango kikubwa huchangiwa na Mto Kikuletwa kupoteza mwelekeo wa maji kutokana na kujaa takataka zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu kandokando ya mto huo.

ASILI YA MTO KIKULETWA

Mto Kikuletwa ni mojawapo kati ya mito iliyopo nchini katika eneo la Kaskazini Mashariki. Kama ilivyo kwa baadhi ya mito mingine inayopatikana katika ukanda huo, unatiririka hadi Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Maji yake yakifika Bwawa la Nyumba ya Mungu, safari yake haiishii hapo, maji huendelea kutiririka moja kwa moja hadi Bahari ya Hindi kupitia Mto Pangani.

WANANCHI WANAZUNGUMZIAJE MAFURIKO?

Mmoja wa wakazi wa Mikocheni, katika eneo hilo, Erasmus Makule, anasema kama serikali itaweka mikakati ya kudumu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itasaidia maji kuwa na manufaa hasa kwa wakulima.

Makule anasema katika kipindi cha mvua mto ukifurika watoto wake wawili ambao wanasoma Shule ya Langasani na Sekondari ya TPC wanashindwa kuhudhuria masomo kutokana na mafuriko.

“Adha si kwetu pekee hata hawa wafanyakazi wa TPC mara kadhaa wameshindwa kwenda kazini kutokana na barabara hazipitiki kwa mafuriko yanayotokana na kuvunjika kwa kingo za mto huo pamoja na uhalisia wa eneo lenyewe kuwa ni tambarare,” anasema Makule.

Fansisca Ulomi, mkazi wa Arusha Chini, anasema tatizo hilo la mafuriko limekuwa la muda mrefu hali inayowafanya kushindwa kuzalisha kwa tija kwa kuhofia mafuriko na hivyo kuendelea kuwa masikini.

Diwani wa Arusha Chini, Leonard Waziri anasema pindi mafuriko hayo yanapotokea mawasiliano hukatika kutoka upande mmoja na mwingine jambo ambalo ni adha kwa wakazi wa kata hiyo.

Anasema kukatika kwa mawasiliano hayo husababisha wananchi kushindwa kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya TPC na badala yake wamekuwa wakilazimika kwenda kupata huduma hiyo katika hospitali ya jirani iliyopo wilayani Simanjiro.

Waziri anasema mbali na wagonjwa bado kumekuwepo na adha kwa wanafunzi hususani wanaotoka katika vijijini vya Mikocheni kushindwa kufika Sekondari ya TPC pamoja na wafanyakazi wa TPC kushindwa kufika kazini kwa wakati.

Marekebisho ya maeneo mbalimbali ya Kiwanda cha Sukari cha TPC yaliyoathirika na mafuriko katika kingo za Mto Kikuletwa, Kata ya Arusha Chini, iliyopo Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro, yakiendelea.

Waziri anasema hadi sasa jitihada zilizochukuliwa ni pamoja na kuwaomba kiwanda cha TPC kuwapatia mitambo ikiwemo katapila kwa ajili ya kusafisha mto huo.

Anasema kwa mara kadhaa TPC wamekuwa wakijitolea kusafisha mto huo na kwa sasa ipo haja kwa serikali yaani halmashauri kutafuta suluhisho la kuondokana na kadhia hiyo.

Mkurugenzi wa Bonde la Maji la Pangani, Segule Segule, anasema kilio cha watu wa ukanda wa tambarare tayari kinafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuacha kuendesha shughuli zao kandokando ya kingo za mto huo.

“Ni kweli suala la mafuriko limekuwa ni tatizo na hii nikutokana na baadhi ya wananchi kuendelea kulima maeneo ya vyanzo vya Mto Kikweleta, tunaendelea kutoa elimu ili wananchi waache kuendesha shughuli kandokando ya kingo za mto na kwa kuanzia tumeanza kuweka alama za utambuzi wa kingo,” anasema Segule.

Jaffary Ally, Ofisa Tawala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC kilichopo eneo hilo la tambarare, anasema mafurikio hayo yamekuwa yakiwasababishia matatizo ya mara kwa mara pamoja na kuathiri nguvu kazi ya wafanyakazi na rasilimali zao.

“Tumeona ni muda mwafaka sasa kuanza kukabiliana na tatizo halo, kwa kuwa linajitokeza kila mwaka na kuathiri wafanyakazi na shughuli za uzalishaji mali ambapo kiwanda cha TPC kimetenga zaidi ya Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa tuta na kusaidia uanzishaji wa skimu.

TPC tumeona ukubwa wa tatizo hili ambalo mbali na kuathiri jamii  inayotuzunguka pia hata sisi humu ndani tumekuwa ni waathirika wakubwa hususani kipindi cha mvua za masika,” anasema Ally.

“Tatizo hili la mafuriko sisi TPC tumeibadili kuwa fursa hivyo tunaenda kuanzisha skimu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambapo pia ni fursa hususani kwa vijana,” anasema Ally.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi anasema aina hiyo ya ubunifu ni fursa kwa vijana katika kuwawezesha kujiajiri kupitia sekta ya kilimo ambapo pia kutaenda kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

“TPC wameonesha kuwa hakuna jambo linaloshindikana kama dhamira ikiwepo ila kukamilika kwa skimu hii ni dhahiri vijana wataenda kupata sehemu sahihi ya kujiajiri,” anasema.

WAZUNGUMZIA KUNUFAIKA NA MRADI HUO

Mkazi wa Kata ya Arusha Chini, Silvester Lyaruu, alisema mafuriko hayo yamekuwa chanzo cha tatizo la njaa kwa wananchi walio wengi wa maeneo ya tambarare na kuiomba serikali kupitia tume ya taifa ya umwagiliaji kuwajengea mabwawa makubwa ya maji yatakayosaidia wakati wa mafuriko.

“Tunatambua vyema wenzetu kiwanda cha sukari kimejizatiti katika kuhakikisha kinawasaidia wananchi wa maeneo ya tambarare katika kujenga tuta kuwa katika kingo za Mto Kikuletwa ili kusaidia hasa nyakati za mvua, ila si vibaya na serikali kuwawekea wananchi mazingira bora,” anasema Lyaruu.

Naye Halima Iddy anakipongeza kiwanda cha TPC na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuishi kwa amani nyakati za masika.

“Tumekuwa kama wakimbizi katika nchi yetu wenyewe, mvua za masika zinapokaribia tunaanza kuuza baadhi ya vitu au kuhamisha kupeleka kwa ndugu, watoto wetu wadogo nao tunawatafutia maeneo ya kukaa ili kujiandaa na mafuriko endapo yatatokea lakini kwa mwanzo huu bora ulioanzishwa na TPC unatuhakikishia usalama wetu,” anasema Halima.

Kamili Mbando ni Diwani wa Kahe Mashariki, eneo lake pia hukumbwa na mafuriko. Anasema mafuriko hutokana na jiografia ya eneo walilopo.

“Mvua hunyesha milimani na maji mengi hushuka pamoja na magogo, kutokana na maeneo ya juu mengi ni mlima ukiwemo na Mlima Kilimanjaro,  hivyo maji yale hushuka na kuvunja kingo za mto hali inayosababisha maji kusambaa kwenye mashamba ya watu, kuharibu mazao na kusababisha njaa.

“Serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia wakulima mbinu na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabwawa maalumu ili maji yale yatumike kwenye kilimo na kunyanyua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” anasema Mbando.

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x