WAKAZI wa Mtaa wa Lulanzi, wilayani Kibaha, mkoani Pwani wameiomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Kibaha kuwapatia huduma ya maji ya uhakika waepuke changamoto ya kukesha kusubiri maji usiku.
Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili walisema maji yamekuwa hayatoki na hata yakitoka ni kidogo na hutoka usiku wa manane.
“Huwa tunaamka usiku sana saa nane, tisa au 10 kwa ajili ya kuchota maji kwa kweli tunataabika sana hili suala la maji kwetu ni changamoto sana tunaomba Dawasa wasikie kilio chetu juu ya suala la maji,” alisema Edina Mdungu.
Ibrahim Kachonga alisema wanashangaa kuona baadhi ya maeneo jirani yakipata maji tofauti na wao.
Meneja wa Dawasa Kibaha, Alfa Ambokile alisema kuwa eneo hilo na baadhi ya maeneo yana mgao wa maji lakini wanakabiliana na hali hiyo kwa kuwa na mradi mkubwa.
Ambokile alisema kuwa hivi sasa wanatekeleza mradi mkubwa wa Pangani ambao utaondoa changamoto hiyo kwani utatoa maji mengi na kero hiyo kukoma.
Alisema mradi huo pia utahusisha ujenzi wa matangi ya kuhifadhia maji yanapokatika ili kero hiyo isiwepo tena kwani maji yatakuwa ya kutosha.