Wakenya waombwa kuiga mfano wa Samia, kutafuta maridhiano

J UMUIYA ya Amani na Maridhiano Tanzania imewashauri viongozi na wanasiasa wa Kenya kuiga mfano wa utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan na kutafuta maridhiano ili kuliepusha Taifa hilo na machafuko.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhad Musa Salum wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandamano yaliyosababisha vurugu, uharibifu wa mali na kuondosha amani nchini Kenya.

“Kwanza tunatoa pole kwa wananchi na serikali ya Kenya kwa madhara yaliyotokea na uharibifu wa mali. Tunawaomba Wakenya katika kipindi hiki watangulize utaifa mbele,” alisema.

Alisema katika maandamano yaliyofanyika Jumatatu ya wiki hii nchini Kenya, kulitokea uharibifu wa mali, kuchomwa nyumba za ibada ukiwemo msikiti na kanisa jambo ambalo linapaswa likemewe na kuzuiwa lisiendelee.

“Kenya ni wenzetu wana Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wanapokosa amani wanaweza kutuambukiza au kuleta wakimbizi tusingependa kufikia huko. Tunatoa wito kwa serikali na wanasiasa waone namna ya kutafuta maridhiano ya kweli na amani endelevu.

Watangulize utaifa kabla ya udini na ukabila,” alisisitiza. Alimshukuru Rais Samia kwa kusimamia vyema maridhiano baina ya serikali na vyama vya siasa na kuitaka Kenya iige mfano huo ambapo Tanzania hadi leo ina maridhiano ya kweli na siasa zinafanyika kwa amani nchini.

“Tunawaomba wauone huu mfano ili na wao wafurahie keki ya amani ya nchi yao.

Kwa sababu ukosefu wa amani madhara yake ni makubwa. Tunaomba waone thamani ya kuwa na amani. Kenya ni nchi moja na Wakenya wataendelea kuwa wamoja,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Maridhiano nchini, Israel Ole Gabriel Maasa aliwataka Wakenya waone amani ni kubwa kuliko cheo chochote kile na pia maslahi ya Taifa ni bora kuliko maslahi binafsi. “Naomba viongozi wa Kenya na wanasiasa walione hili.

Maslahi binafsi yasiharibu amani ya Taifa au sura.

Mazungumzo yana faida kuliko maandamano. Wakae pamoja na kufikia maridhiano. Aidha, Jumuiya hiyo iliwataka Waislamu na Wakristo ambao wote kwa sasa wako kwenye ibada ya kufunga, kuwaombea viongozi wa Tanzania wakiongozwa na Rais Samia ili waliongoze vyema Taifa.

Habari Zifananazo

Back to top button