Wakili ajitoa kesi ya Makonda

WAKILI wa mfanyabiashara, Patrick Kamwelwe katika kesi ya tuhuma za uporaji wa gari aina ya Range Rover inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda na William Malecela (Le Mutuz), Kungh’e Wabeya amejitoa kukusimamia kesi hiyo.

Wabeya amejitoa wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate anayesikiliza kesi hiyo.

Akiwasilisha ombi hilo, Wabeya alidai amefikia uamuzi huo kwa sababu amekosa maelezo sahihi kutoka kwa mteja wake kuhusu uendeshaji wa kesi hiyo.

Advertisement

Alidai kuwa amekuwa akiwasiliana na mteja wake huyo lakini hapati majibu kwa wakati.

Pande zote zilikubaliana na hakukuwa na pingamizi na mahakama iliridhia kujiondoa kwake na kuhairisha kesi hiyo hadi Januari 31 mwaka 2023.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imepanga Januari 31 mwaka 2023 kusikiliza upande mmoja maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa Makonda na Malecela kutokana na upande wa mlalamikaji kushindwa kuwasilisha mahakamani kiapo kinzani ndani ya siku 14 uliopangwa kisheria.

Katika maombi hayo mawakili wa mjibu maombi wameiomba mahakama kutoa amri ya Kamwelwe kuwasilisha dhamana ya kesi yake itakayoweza kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo ikiwa ameshindwa katika kesi hiyo.

Katika kesi hiyo mfanyabiashara Patrick Kamwelwe alifungu kesi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda na Malecela akidai alipwe fidia ya zaidi ya Sh milioni 240 ambazo ni gharama za kodi ya thamani ya gari hilo la kifahali.

Katika hati ya madai ya mfanyabishara huyo anadai kuwa yeye na Lemutuz ni marafiki na alitumia urafiki wake kumkabidhi Makonda gari aina ya Range Rover.

Mfanyabiashara huyo anadai alimkabidhi gari hilo Lemutuz ili ampatie Makonda aweze kutumia wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa makubaliano alitumie kwa wiki mbili na kisha amrudishie.

Lakini ilikuwa tofauti na makubaliano hayo ambapo Makonda aliendelea kulitumia gari hilo na mpaka sasa halijarudishwa kwake kama mmiliki.