WAKIMBIZI wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Nduta Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, wametakiwa kuwekeza nguvu na akili zao katika kufikiri kurudi nchini kwao.
Mkurugenzi wa Idara ya wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Sudi Mwakibasi alisema hayo akizungumza na wakimbizi wa Burundi kwenye kambi hiyo wakati wa uzinduzi wa kituo cha kutoa huduma za afya ya msingi na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kinachoendeshwa na Shirika la Medical Team International.
Mwakibasi alisema kwa sasa Burundi ina amani na watu wengi wamekuwa wakifanya kazi zao za maendeleo, hivyo haiingii akilini kuona kuwa bado wapo watu wengi wa nchi hiyo wanahifadhiwa kwenye makambi nchini kama wakimbizi.
“Serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa tumekubaliana wakimbizi warudi kwao kwa hiari baada ya kujiridhisha uwepo wa amani ya kutosha lakini bado idadi ya wakimbizi wanaojiandikisha kurudi ni ndogo sana, hali hii itachukua muda mrefu wakimbizi kurudi kwao,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema pamoja na kuboreshwa kwa baadhi ya huduma kutokana na hali ya kibinadamu, lakini mashirika mengi hayataendelea kutoa huduma kambini humo kwani kwa sasa wakimbizi hao hawana hadhi ya kuwa wakimbizi kutokana na nchi yao kuwa na amani.
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi rasmi wa kituo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Medical Team International (MTI), Dk George Mwita alisema uzinduzi wa kituo hicho cha matibabu unaangazia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ambayo yamekuwa na uhitaji wa kupata huduma maalumu.