Wakimbizi wagoma kurejea Burundi, wataka waende Ulaya
LICHA ya WAKIMBIZI wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma kutokuwa na sifa ya kwenda nchi ya tatu, wakimbizi hao wamegoma kurudi nchini kwao na kubuni njia mbadala itakayowawezesha kwenda Ulaya na Marekani.
Mkurugenzi wa Idara wa wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi amesema kuwa baada ya kukosa sifa ya kwenda Ulaya na Marekani wakimbizi wamejiingiza kwenye mahusiano ya kufunga ndoa na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo waliopo kwenye kambi hiyo, ili waweze kutimiza kusudio lao.
Akizungumza mbele ya ujumbe wa serikali ya Burundi unaotembelea kambi za wakimbizi za Nyarugusu wilayani Kasulu na Nduta Wilaya ya Kibondo, Mwakibasi amesema kuwa sifa pekee ya wakimbizi wa Burundi waliopo kwenye makambi mkoani Kigoma ni kurudi nchini kwao.
Mkurugenzi huyo amesema baada ya mkutano wa mashauriano wa pande tat, ambao ni Serikali ya Tanzani, Burundi na Shirika la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), wamekubaliana kuwaondoa wakimbizi hao wa Burundi kutoka kwenye kambi ya Nyarugusu Wilaya ya Kasulu na kuwahamishia kambi ya Nduta Wilaya ya Kibondo.
Awali Kaimu Mkuu wa kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Humphrey Mrema alisema kuwa zoezi la wakimbizi kujiandikisha kurudi kwao kwa hiari linasuasua, ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Julai ni wakimbizi 405 wa Burundi walijiandikisha na kurejeshwa kwao.
Mrema Akielezea suala la wakimbizi wa DRC wanaopelekwa nchi ya tatu, amesema kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Julai mwaka huu wakimbizi 4,584 wamenufaika na suala hilo, ambapo kati yao wakimbizi 4,371 walipelekwa Marekani, 185 wameenda Canada, 18 Australia ambapo wakimbizi 10 wameenda Finland na Ufaransa.
Akizungumza kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Maendeleo ya Jamii wa Burundi,Calinie Mbashurimana amesema kuwa ndoa wanazofunga wakimbizi hao ni za aibu, kwa sababu hazina hadhi kwa tamaduni zao na wengi wameoa au kuolewa kwa tamaa ya kupata kitu, badala ya mapenzi ya moyo ,hivyo watatumia nafasi yao kwenye ziara hiyo kuwashawishi warundi Burundi.