Wakongwe chali, wapya wapeta uchaguzi CCM

Katibu wa Hitikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akitangaza majina ya wenyeviti wa wilaya waliopitishwa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka hadharani majina 550 ya wanachama wake waliopitishwa kugombea nafasi za uenyekiti ngazi ya wilaya huku sura mpya zikichomoza na wakongwe kukatwa.

Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka aliyoitoa saa 9: 14 usiku kuamkia le oleo, Jumatano, maeneo mengi nafasi hizo zinawaniwa na wanasiasa chipukizi ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo sura zimekuwa zikijirudia.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, vigogo ambao walikuwa wakipigiwa chapuo kutetea nafasi zao majina hayajarudi
ni Ubaya Chuma aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Ilala, Mishi Alhazar aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Temeke na Harold Maruma (Kinondoni).

Advertisement

Naye na Mussa Kilakala ambaye Mwenyekiti UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam naye ameangukia pua baada ya kujitosa kuwania uwenyekiti wilaya ya Ilala na jina lake kukatwa.

Katika taarifa hiyo ya Shaka inaonyesha kwa upande wa Ilala jina la kigogo lililochomoza ni la Assa Simba Haroun ambaye ameshawahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala lakini hakumaliza ngwe yake baada ya mwaka 2017 kuvuliwa uanachama.

Katika sakata hilo, Assa na wenyeviti wengine akiwemo Sophia Simba walifukuzwa uanachama na kikao cha NEC baada ya vuguvugu la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, mwaka 2020 alisamehewa na kurejeshewa uwanachama wake ambapo alijitosa kuwania ubunge Jimbo la Segerea na kushika nafasi ya pili, Bonna Karua akiibuka kidedea.

Naye katibu Mwenezi wa CCM Ilala, Said Sultan Sidde Salima Hamisi Hilary ni sura ngeni katika medali ya siasa za Ilala.

Kwa upande wa Kinondoni waliopita ni Kassim Shabani Kavitenda, Pilly Athuman Chande ni sura mpya zilizopenya kwenye kinyang’anyiro, huku Shaweji Abdallah Mkumbura akiwa ni mkongwe pekee aliyepita.

Katika taarifa hiyo, wilaya chache majina yamepelekwa manne lakini maeneo mengi wameteuliwa watu watatu wanawake wakichomoza maeneo mengi.

Uchaguzi wa wenyeviti wa CCM ngazi ya wilaya umepangwa kufanyikia ndani ya siku mbili ambazo ni Oktoba Mosi na 2, 2022 nchini kote ili kuruhusu mchakato wa ngazi ya mkoa mwishoni mwa Oktoba.

Majina ya Wenyeviti wa Wilaya waliopitishwa