Wakubaliana kupangisha ofisi kulipa deni la ujenzi la mil 7.4/-

Wakubaliana kupangisha ofisi kulipa deni la ujenzi la mil 7.4/-

WANANCHI wameridhia jengo la Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Muhalitani Tandale mkoani Dar es Salaam, lipangishwe ili ipatikane fedha ya kulipa deni la vifaa vilivyotumika kujenga ofisi hiyo lenye thamani ya Sh milioni 7.4.

Hayo yalibainika katika mkutano wa wananchi ulioitishwa kwa ajili ya kuzungumzia changamoto mbalimbali zilizopo katika mtaa huo ikiwemo ya ulinzi na usalama.

Akiwakilisha wananchi wengine wa eneo hilo, Ally Moge alisema kwa kuwa deni hilo ni la miaka miwili sasa na mhusika aliyetoa vifaa vya ujenzi ili kukamilisha jengo hilo anahitaji fedha zake ni bora kwa sasa jengo hilo likapangishwa ili ipatikane fedha za kulipia deni hilo.

Advertisement

“Tunaomba jengo hili lipangishwe baada ya deni kuisha lirudi kwa wananchi. Funga ofisi pangisha deni likimalizika tutarudi,” alisema.

Hatua ya wananchi hayo imefikiwa baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Sudi Makamba kuitisha kikao kinachozungumzia changamoto mbalimbali na kuweka bayana kuhusu deni hilo ambalo limekuwa linamnyima amani baada ya halmashauri kusema kuwa haina bajeti ya kulipa fedha hizo.

Katika kikao hicho, Makamba alisema kabla ya ujenzi wa ofisi hiyo alijitahidi kutoa taarifa katika ngazi zote zinazostahili na kupata baraka za ujenzi wa jengo hilo.

Alisema mpaka ujenzi huo kukamilika wananchi walichanga Sh milioni 1.5, nyingine zilipatikana kwa kukopa vifaa vya ujenzi kutoka kwa wadau, deni ambalo halijalipwa.

“Hata fedha ya kulipa pango shilingi 48,000 iliyokuwa ikitolewa na halmashauri hivi sasa siipati kwa takribani mwaka mmoja sasa, fedha ambayo ingesaidia pia kupunguza deni hili lililopo. Nimelileta kwenu ninyi mlinituma na kunitaka nisimamie ujenzi wa ofisi hiyo,” alisema.

Katibu wa CCM Kata ya Tandale, John Mbele aliwataka wananchi kutumia busara wakati taratibu zikifuatwa za kukodishwa jengo hilo ili zipatikane fedha ya kulipa deni.

“Kwa kuwa mkurugenzi halitambui, Ofisa Mtendaji wake anayelitumia jengo hilo naye atafute ofisi ya kutumia. Naunga mkono mapendekezo ya wananchi kukodishwa kwa jengo hilo ili kurudisha pesa iliyokopwa,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Tawi la CCM Muhaliltan Tandale, Hassan Sagheir alitoa pole kwa mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa na kumtaka afuate taratibu za kisheria ili jengo hilo likodishwe kufidia deni hilo.

“Kabla ya kuja hapa viongozi walikaa kwenye eneo la baa ijulikanayo kama toroka uje, kukawa na maneno mengi kuwa viongozi wanakaa baa sasa jengo limepatikana danadana zinakuwepo, bora lipangishwe fedha irudishwe kwa aliyekopwa vifaa vyake,” alisema Hemed Singano.

Mkuu wa Kituo cha Polisi, Kata ya Tandale, Kazumba Sika aliwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati suala hilo linashughulikiwa.

Mtendaji wa mtaa huo, Nemes Peter aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati jambo hilo linashughulikiwa