Wakulima 200 kunufaika mradi wa kilimo rafiki Geita

GEITA: WAKULIMA 200 wa halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani hapa wamepewa fursa ya kunufaika na mradi wa Kilimo Rafiki unaolenga kuhamasisha matumizi ya njia za asili ili kufikia uzalishaji wenye tija.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Kijani Consult Tanzania kwa kushirikiana na shirika la DIB Dernmark chini ya ufadhili wa shirika la CISU Dernmark kwa kutoa elimu kupitia mashamba darasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kijani Consult Tanzania, Mandolin Kahindi ametoa taarifa hiyo Agosti 20, 2025 katika hafla ya kugawa mbegu zilizothibitishwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) katika kijiji cha Lwamugasa.
Amesema mpaka sasa kuna mashamba darasa kwenye kata ya Nyaranzwaja, kata ya Kagu na kata ya Nyakagomba na kila kata kuna vijiji viwili, sawa na jumla ya vijiji sita ikihusisha wakulima 180 na wakulima viongozi 12.

“Pia kwenye kila kijiji kuna shamba darasa ambalo kila mkulima anachangia kwenda kulima wakipata huo ujuzi wanaenda kutekeleza pia kwenye mashamba yao wenyewe”, amesema Kahindi.
Kahindi amesema dhamira kuu ya mradi wa Kilimo Rafiki ni kuhamasisha, kuelimisha lakini pia kutangaza fursa kwenye maeneo ya kilimo biashara sambamba na uhifadhi wa mazingira na maliasili na utalii.
Amesema mradi pia utawasaidi wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kupitia mashamba darasa kwa kufuata kanuni bora za kilimo, matumizi ya mbolea za asili na njia bora za kuhifadhi mazao.

Ofisa Kilimo kata ya Nyakagomba, Benjamine Faustine amekiri uwepo wa kilimo cha mazoea imekua chanzo cha wakulima wengi kutumia raslimali nyingi kuandaa mashamba na kuambulia mavuno kidogo.
Faustine ameahidi kusimamia mradi wa Kilimo Rafiki uweze kuzaa matunda kwa wanufaika kwa kuwa umejikita katika njia za asili ambazo kila mkulima wa kawaida anamudu kuzifuata kwa maslahi mapana.
Mkulima Kiongozi, Isack Zabron amekiri ulimbukeni wa matumizi ya kemikali na mbolea za kisasa bila muongozo sahihi imewafanya kuwa wategemezi wa mbegu, pembejeo na viuatirifu kwa kila mwaka.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakagomba, Ladisilaus Alex amesema kuwa mradi wa Kiimo Rafiki unaenda kuleta mapinduzi ya kilimo kwa kuachana na kilimo cha matuta ili kutumia eneo dogo kuzalisha zaidi.



