WAKULIMA wa mazao mbalimbali mkoani Kagera wamefanya maandamano ya amani yanayolenga kumpongeza Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kutoa mbolea ya Ruzuku kwa bei nafuu ambayo wanaweza kuimudu na kupandia mazao yao.
Wakulima zaidi ya 400 walioandamana mpaka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kagera walikuwa na na ujumbe usemao “Ahsante mkombozi wetu mama Samia ulipo wakulima tupo ,na mabango mengine yalisema “Tunamuombea mtoto wetu msamaha ambaye alisomeshwa kwa fedha ya wakulima asituchonganishe na mama yetu mpendwa ”
Wakulima hao walipokelewa na mkuu wa Mkoa na kuwasilisha sifa lukuki za mabadiliko mbalimbali katika bei za mazao yao mfano kahawa, kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 3,000 kwa kilogramu moja, mbolea kutoka shilingi 150,000 hadi 70,000 na kudai kuwa hiyo ni hatua njema na kubwa katika ukombozi wa wakulima.
Akisoma lengo la maandamano hayo Josephati Joseph ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Kata Kahororo kwa niaba ya wakulima alisema kuwa anaaamini maandamano hayo ya amani yatajenga umoja na mshikamano kati ya wakulima, serikali na wanasiasa ambao wanatambua hakuna mchango wowote ulipo katika sekta ya kilimo tangu Rais Samia alivyoingia madarakani.
“Tunapiga magoti na kuomba radhi kwa watoto ambao wanaingia katika siasa na kuonyesha utovu wa nidhamu wa kutuchonganisha wakulima na serikali yetu, Rais Samia amefanya makubwa ambayo hatujawai kuyategemea ,mabadiliko katika bei za kahawa ,kwa sasa Mpaka wa Kyerwa unapokea wafanyabiashara kutoka Sudani ambao wananunua ndizi, tulizuiliwa huko nyuma.
“Kwa sasa Mkoa wa Kagera unapata mbolea ukilinganganisha na miaka ya nyuma hakuna kama mama Samia alipo wakulima tupo nyuma “alisema Joseph.
Nae Mkuu mkoa Kagera Alberth Chalamila, amewahakikishia wakulima kuwa atawasilisha pongezi zao kwa Rais wao na kudai kuwa anawakaribisha kuwasilisha kero zao zinazowakabili wakulima kwa mamlaka zinazohusika kuliko kuongelea vijiweni na kuiteta vibaya serikali ambayo inawasaidia.
Aidha alisema kuwa kiwanda cha mbolea kikubwa nacho kitakuwa na mbolea ya kupandia mazao kukuzia kimeanza kujengwa mkoani Kagera na wakulima wategemee siku zijazo kupata mbolea kwa bei nafuu sana.