Wakulima Kongwa wakabidhiwa trekta 15

MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Remidius Emmanuel amekabidhi trekta 15 kwa wakulima wilayani humo katika hafla fupi iliyoandaliwa na Kampuni PASS Leasing kwa kushirikiana na Agricom Africa Limited katika Mamlaka ya Mji mdogo Kibaigwa.

“Kukopa trekta ni jambo moja, kulifanya trekta kuleta tija ni jambo lingine, hivyo nawashauri wakulima kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya matumizi ya matrekta haya ili tija iweze kuonekana hatua itakayowasaidia kurejesha mikopo yao kwa wakati. Bado serikali tutaendelea kutoa ushirikiano wa kitaalamu kwa wakulima wote ili ufanisi uweze kuonekana,” alisema.

Aliipongeza Kampuni ya PASS Leasing ambayo ni  kampuni tanzu ya PASS Trust kwa kuwa moja ya taasisi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuendeleza uwekezaji katika sekta ya kilimo na kutoa dhamana kwa mikopo ya kilimo kupitia benki hapa nchini.

Wakati huohuo, Mkuu huyo wa Wilaya amezindua mradi wa maji katika Shule ya Msingi Mkwala, Kata ya Ugogoni.

Mradi huo wenye thamani ya Sh 37,212,000 ukihusisha gharama za uchimbaji wa kisima na miundombinu ya maji pamoja na mfumo wa kuvuna maji ya mvua shuleni hapo umefadhiliwa na Parishi ya Crock Ham Hill kutoka Uingereza.

Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuondoa tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa huduma ya  maji shuleni hapo, hatua inayotazamiwa kuongeza utulivu wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuboresha usafi wa mazingira.

“Maji ni uhai, matarajio yangu ni kwamba shule hii sasa inaenda kuwa kielelezo katika nyanja zote ikiwa mnyororo wa maji haya utatumika kikamilifu na kuleta tija, ninayo imani kubwa na uongozi wa shule hii pamoja na kijiji hiki,” alisema.

Mradi huo ni matokeo ya mahusiano mazuri baina ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa na Wafadhili wa Mradi huo, Parishi ya Crock Ham Hill (Dayosisi ya Rochester) kutoka Uingereza.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button