Wakulima kupewa elimu kilimo tija

HALMASHAURI ya Wilaya ya Morogoro imeweka mkakati endelevu wa kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo kwa ajili ya utoaji elimu za ugani kwa wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji wenye tija wa mazao mbalimbali wakiwemo ya viungo na kuiingizia mapato ya kutosha halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Joanfaith Kataraia amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ya kiasi cha jumla ya Sh bilioni 52.4.

Kiasi hicho cha fedha kitatokana na makusayo ya mapato ya ndani Sh bilioni 6. 5 pamoja na fedha kutoka serikali kuu ambayo ni ruzuku ya jumla ya Sh bilioni 45.9 kwa ajili ya mishahara, miradi ya maendeleo na fedha za matumizi mengineyo.

Amesema halmashauri hiyo inategemea mapato yake kutokana na mazao ya kilimo ,hivyo kwa mwaka ujao wa fedha (2024/2025) imeweka fedha za kutosha kwa ajili ya kuiendeleza na kuiboresha sekta hiyo na nyingine zimeelekezwa kwenye sekta ya elimu , afya , viwanda na biashara .

“ Tumejipanga kukusanya fedha hizi za mapato ya ndani kwa sababu tumejiwekea mikakati kama halmashauri kwenye kuwekeza zaidi kwenye kilimo “ amasema Kataraia .

Kataraia pia amesema fedha hizo zimelenga pia kutumika katika miradi ya maendeleo , vikundi vya akina mama, vijana na wenye ulemavu na matumizi mengineyo.

“ Kwenye kilimo tumepanga kutoa elimu kwa wakulima kufanya kilimo cha kisasa , kutumia zana sahihi kwenye kilimo na mkakati upo zaidi kwenye mazao ya viungo yakiwemo karafuu , adalasini na mengineyo” amesema Kataraia.

 

Amesema halmashauri imeweka nguvu kwenye zao la michikichi licha ya kuwa ni la muda mrefu kidogo lakini inaamini litaleta tija kubwa zaidi katika kukuza uchumi wa wananchi na halmashauri yenyewe.

“ Tunawashawishi wananchi walime michikichi ili waweze kujitengenezea kipato chao na halmashauri kupata fedha za makusanyo “ amesema Kataraia .

Katika uanzishaji wa vyanzo vipya vya mapato ,amesema halmashauri imeweka mpango wa kujenga jengo la kisasa la kitega uchumi eneo la Kata ya Mvuha yaliyopo makao makuu wa halmashauri ili kuongeza mapato yake.

Ametaja mkakati wingine ni wa kujenga machinjio ya kisasa kupitia sekta ya mifugo licha ya kuwa na eneo zuri ya kuchinja mifugo na kupata nyama safi , hatua hiyo itaiwezesha halmashauri kuwa na chanzo kipya cha ukusanyaji wa mapato.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema halmashauri itaendelea kusimamia makusanyo na kuziba mianya yote ya utoroshaji wa bidhaa mbalimbali pasipo kulipia mapato yake .

“ Tunauhakika hadi kufika mwaka 2025 tutakuwa tumekusanya kiasi hiki cha fedha Sh bilioni 6.5 na kuboresha huduma za jamii “ amesema Kataraia.

Habari Zifananazo

Back to top button