Wakulima kutatuliwa changamoto kidigitali

DAR ES SALAAM; WAKULIMA na wajasiriamali watanufaika na ukuaji wa teknolojia sambamba na kutatuliwa changamoto zinazowakabili kwa kutumia bidhaa mbalimbali za kidijitali zitakazoibua masoko mapya mijini na vijijini na kuongeza mapato.

Akizungumza wakati wa utilianaji saini mkataba wa miaka mitatu kati ya Kampuni ya Airtel na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Frank Nyabundege amesema ubia huo unalenga kukuza ukuaji sekta ya kilimo.

“Ushirikiano huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yatakayowagusa wakulima wote nchini Tanzania,” amesema Nyabundege.

Advertisement

Amesema ushirikiano huo unakwenda na mikakati ya serikali ya kuunga mkono juhudi za wadau wa kilimo kwa kupambana na changamoto mbalimbali ndani ya sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kifedha kama ilivyotajwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wa wadau wa COP28 uliofanyika Desemba 4, 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel, Dinesh Balsingh amesema kwa kushirikiana na TADB wanadhamira ya dhati ya kusaidia Watanzania kupitia ubunifu katika sekta ya mawasiliano.

“Hii ni kwakua tunaamini wakulima wanastahili kuwa miongoni mwa vikundi vinavyotakiwa kunufaika na ukuaji wa teknolojia nchini. Hivyo, Ushirikiano wetu na TADB unalenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima,” amesema.