Wakulima mil 3.7 wasajiliwa mfumo wa mbolea ya ruzuku

DAR ES SALAAM: ZAIDI ya wakulima milioni 3.66 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidijiti wa mbolea ya ruzuku nchini hadi sasa na katika msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2023/24 tayari wakulima 521,518 wamepata mbolea ya ruzuku.

Akizungumza na HabariLEO jana, Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Louis Kasera alisema mbolea ya ruzuku imeanza kusambazwa kwa wakulima.

Alisema hadi sasa wakulima 3,664,942 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidijiti wa mbolea ya ruzuku nchi mzima na kazi la usajili ni endelevu katika mikoa yote na kuwataka wakulima waendelee kujisajili ili kunufaika na mbolea ya ruzuku.

Aidha, alisema katika msimu huu mpya wa kilimo wa mwaka 2023/24 mikoa ambayo imeshaanza msimu umeanza zaidi ya wakulima 521,518 wamenunua mbolea ya ruzuku kulingana na mahitaji yao na kuwa idadi zaidi itaendelea kulingana na mahitaji.

“Msimu wa kilimo umeanza, na mbolea ya ruzuku imeshaanza kusambazwa maeneo tofauti nchini na TFRA imeshasajili vituo vya usambazaji mbolea zaidi ya 5,223, hii inajumuisha na vituo vya vyama vya ushirika itakavyotumika kusambaza mbolea nchini katika msimu huu,” alisema Kasera.

Kuhusu shehena ya mbolea iliyopo nchini hadi sasa na mahitaji halisi kwa msimu huu, Kasera alisema hadi Oktoba mwaka huu jumla ya tani 650,356.29 za mbolea sawa na asilimia 76.61 ya mahitaji ya mbolea na virutubisho vyake nchini.

Kasera alisema mahitaji ya mbolea na virutubisho vyake yanakadiriwa kufika tani 848,884 katika msimu wa kilimo wa 2023/24.

Septemba 8, mwaka huu bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliitaka Wizara ya Kilimo kusimamia kwa ukamilifu ugawaji wa mbolea kwa wakulima ikiwamo kuongeza vituo vya mauzo na kuboresha mifumo ya upatikanaji wa mbolea.

Alisema serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kuwapunguzia makali ya bei ya pembejeo hiyo muhimu katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Majaliwa alisema msimu wa kilimo wa mwaka ulioisha 2022/23 matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 538,000 sawa na ongezeko la asilimia 48, ongezeko lililotokana na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ambayo serikali imekuwa ikitoa kuanzia msimu wa kilimo 2022/23.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema katika mwaka 2023/24, kupitia TFRA itaendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea nchini kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima hadi mwaka 2025/2026.

Bashe alisema lengo la serikali kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ni kuongeza matumizi ya pembejeo hiyo muhimu katika kilimo kutoka kilo 19 kwa hekta hadi angalau kilo 50 kwa hekta na kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button