Wakulima milioni 3 kunufaika na mifumo ya chakula Afrika

WAKULIMA milioni tatu nchini watanufaika na mpango mkakati wa shirika linalojishughulisha na ukuaji endelevu wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRA) kwa kupatiwa masoko ya mazao yao.
Akizungumza na HabariLEO baada ya uzinduzi wa mpango mkakati, Meneja wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela alisema kuwa mkakati huo utawanufaisha wakulima milioni tatu nchini kwa kuwapatia masoko ya mazao yao.
Alisema mkakati huo umegawanyika katika maeneo tofauti kijiografia ikiwamo Nyanda za Juu Magharibi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini, Nyanda za Juu Kaskazini na Zanzibar.
Mazao yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na mahindi, mtama, maharage, mihogo, alizeti, soya, ngano, viazi na mazao ya bustani.
Alisema mpango mkakati uliozinduliwa umelenga kuwajengea uwezo vijana na wanawake wa Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa kilimo na hivyo kukuza ajira, ukuaji wa ustawi wa jamii na uchumi.
“Mkakati huo unajumuisha uboreshaji wa upatikanaji wa fedha na masoko na kukuza utumiaji wa teknolojia mahiri za hali ya hewa na matumizi ya pembejeo kama vile mbegu na mbolea,” alisema.
Pia kuwa na jukwaa thabiti la kushirikisha maarifa na ubunifu na kukuza mijadala yenye maarifa kuhusu changamoto katika kilimo na biashara na kuboresha ufikiaji wa afua muhimu za kifedha kwa lengo la kuwezesha matumizi makubwa ya teknolojia na sayansi katika kilimo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema: “Tumetoa milioni 20 kwa binti aliyekuwa akitengeneza mvinyo kwa kutumia nyanya, huyo binti aliibuliwa kwenye maonesho ya Nanenane, alihitaji fedha kwa ajili ya mashine ili aweze kuboresha uzalishaji na kununua malighafi.”
Alisema masoko yatafikiwa kwa uhalisia wake kama kunakuwa na uzalishaji wenye tija.