Wakulima Muheza wataka ushirika kukwepa ulanguzi

WAKULIMA wa mazao ya viungo katika vijiji vilivyopo katikati ya Hifadhi ya Misitu ya Amani na Nilo Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga wameiomba serikali kuanzisha vyama vya ushirika ili kupata bei nzuri ya mazao na kuondoa changamoto ya ulanguzi inayowakabili kwa sasa.

Mazao yanayolimwa katika vijiji saba vinavyonufaika na mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaolenga matumizi bora ya ardhi na utunzaji wa mazingira ni pamoja na Iliki, karafuu, mdalasini na pilipili manga.

Vijiji saba vilivyopo katika ushoroba wa Hifadhi ya Misitu ya Amani na Nilo vinavyonufaika na Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasi ni Zirai, Kizerui, Antakae, IBC Msasa, Shamba Ngeda, Kwendimu na Magoda.

Wakizungumza kwa nyakati mmoja wa wakulima hao mkazi wa kijiji cha Kizerui, Stephano Diwa amesema kwasasa wanauza mazao hayo kila mtu na bei yake kwasababu ya uwepo wa walanguzi.

“Mfano kipindi cha nyuma walikuwa wananunua kilo moja karafuu Sh 9,000 hadi 10,000 na wanauza 15,000 hadi 20,000 wanapata faida wao sisi hatufaidiki na kilimo hicho hivyo tunatumia nguvu nyingi bila faida.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Kizerui, Selina Kusaga ameeleza kuwa wanapata changamoto kuuza mazao kwa bei ya chini ambayo haina tija kwao na wanazalisha mazao hayo mara moja kwa mwaka.

“Tunaendelea kuwa masikini na wengine wanatajirika kupitia sisi hili linatuumiza sana sisi wakulima wa hapa Kizerui na mazao yetu yanasoko nzuri tu huko duniani.

Mkazi wa kijiji cha Antakae,Bertha Maguluko amebainisha changamoto ya uchafuzi wa ubora wa karafuu kwa kuchanganywa na vikonyo hali inayosababisha bei ya karafuu za Tanzania kuonekana kutokuwa na ubora.

“Sisi wakulima tunatenga vizuri karafuu zetu lakini wafanyabishara wanakuja kuchanganya na vikonyo hali inayosababisha kuwa karafuu yetu ionekane kuwa haina ubora kitu ambao sio sahihi kama kukiwa na sehemu moja ya kuuza itakuwa ahueni.

Ameongeza “Tunaomba masoko ya uhakika ya ndani na nje kuwe na wanunuzi maalum wa mazao kuna wakati unashida ya fedha anakuja mtu kuchukua kwa bei rahisi shambani.

Ameomba serikali iingilie kati Serikali inagalie kuwe na ukopeshaji tunaingia majaribuni ,tunapata hasara wala hatuoni faidaa tunaomba ushirika wa kununua viungo vyetu na kutupa mikopo kuna vishoka ambao wanatunyonya sana hasa tukiwa na shida.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Kizerui ,Andrew Kingazi amesema eneo la kilimo hai ni ekari 785.6 maeneo yote ni kilimo hai huku idadi ya watu ikiwa ni 1765.

Ameeleza kuwa tatizo lao kubwa ni kupata soko la uhakika na pia wapo wanaofunga mkataba lakini sio kwa wakulima wote hivyo wangekuwa na mpango wa wakulima wote kama chama cha ushirika ingewakwamua kiuchumi.

“Inawezakana unapata kile ulichopata na unaishia kulipa madeni hatupangi kufanya maendeleo kama kujenga nyumba au maendeleo mengi ni kama bado tumesimama .

Aidha amesema kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wamekuwa wakipata mafunzo ya utunzaji mazingira na kilimo hai na kufanya wakulima kuacha kutumia kemikali na kujua kuweka akiba kupitia vikoba.

“Faida ya kilimo hai ni kubwa na mazao yanasoko kubwa wananchi baada ya kupewa elimu ya kilimo hai wanamwamko mkubwa wa kilimo hai lakini changamoto la soko la uhakika ambapo kwa mwaka huu tumejadili kukutana na wadau ambao tunazungumza ili kuingia katika soko la dunia.

Habari Zifananazo

Back to top button