NAIBU Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde, amewahakikisha wakulima wa kahawa mkoani Kagera kuwa, serikali itaendelea kuwasimamia maofisa ugani kutoa huduma bora kwa wakulima, ili wazalishe kwa tija.
Aliyasema hayo wakati akizindua awamu ya tatu ya kugawa miche 800,000 ya kahawa kwa wakulima Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, imekusudia kuleta mabadiliko chanya kuhakikisha mkulima anapata huduma bora za ugani na kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 300,000 za kahawa Mkoa wa Kagera, ifikapo mwaka 2025.
Alisema serikali imeongeza bajeti ya huduma za ugani kwa mwaka 2022/2023 kutoka Sh milioni 600 hadi Sh bilioni 15, ikiwa pamoja na ugawaji wa pikipiki kwa maafisa ugani wote nchi nzima.
Mwenyekiti wa bodi ya Kahawa nchini, Profesa Aurelia Kamzora, alisema kuwa kuna mabadiliko makubwa katika bei ya kahawa, tangu serikali ya awamu ya sita ilivyoanza kuchukua hatua za kumnufaisha mkulima na kupunguza tozo zisizo na tija.
Alisema miaka ya nyuma, mkulima aliuza kahawa yake kima cha juu ikiwa Sh 1,200 kwa kilo, lakini msimu huu mkulima anauza kilo moja ya kahawa kati ya Sh 1,650 hadi Sh 2,150.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kitalu cha JJAD, Albert Katagira, alisema alisaini mkataba na Bodi ya Kahawa, kuzalisha miche milioni 3 katika awamu hii ya tatu, ambapo miche hiyo inaendea kuzalishwa hadi kufikia Desemba itakuwa imekamilika.