‘Wakulima wa korosho waelimishwe uhuishaji taarifa’
BAADHI ya Wakulima wa korosho mkoani Mtwara, wameiomba serikali kuwapatia elimu ya kutosha wakulima hao juu ya suala la uhuishaji wa kanzidata linaloendelea.
Akizungumza leo mkoani Mtwara katika uzinduzi rasmi wa uhuishaji wa kanzidata ya wakulima wa korosho nchini, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala (TANECU), Karim Chipola amesema suala hilo ni zito na lina umuhimu mkubwa kwa wakulima hao.
Amesema kutokana na umuhimu huo, ipo haja kwa wakulima kupatiwa elimu ya kutosha na isiishe tu ngazi za juu, bali ifike ngazi za chini kupitia maofisa ugani walioko kwenye maeneo yao.
“Elimu ikitolewa kikamilifu kwa wakulima itasaidia kujitokeza kwa wingi kuandikishwa katika zoezi hili, ili kuwezesha pembejeo kufika kwa wakati na kwa mahitaji yanayohitajika,”amesema Chipola
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brigedia Jenerali mstaafu Aloyce Mwanjile, amesema suala la usajili wa wakulima wa zao hilo nchini lilianza mwaka 2018, ambapo wakulima zaidi ya 300,000 walisajiliwa.
Pia liliendelea kwa nyakati tofauti na hadi Desemba 2022 wakulima karibu 400,000 walikuwa wamesajiliwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amewasisitiza wakulima wajitokeze kwa wingi kuhuisha taarifa zao, kwani suala hilo lina lengo la kuongeza uzalishaji wa korosho nchini kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025/26.