Wakulima wa korosho watakiwa kuongeza mazao

WAKULIMA wa Korosho mkoani Mtwara wametakiwa kuhakikisha wanalima mazao mengi zaidi ili ikitokea changamoto ya mavuno kwenye korosho kuwe na zao mbadala la kuwaingizia kipato.

Hayo yamesemwa Jana Mei 10, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas katika Mkutano Mkuu wa 23 wa mwaka 2022/23 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara Cooperative Association (MAMCU) Limited uliyofanyika eneo la Mangaka Wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa.

Kanali Ahmed Abbas ameshauri kwa mwaka ndani ya mifuko ya wakulima hao kuwe na fedha ambayo inatokana na uwepo wa mazao mengine katika Wilaya na Mkoa kwa ujumla. Hata hivyo ameutaka uongozi wa ushirika huo kutimiza wajibu katika kuwahudumia wakulima kwa kutenda haki.

Aidha, MAMCU kwa msimu unaoishia wa 2022/23 imezalisha korosho tani 59,600 zenye thamani ya Sh bilioni 111.4 sawa na asilimia 66.0 ambapo mkoa ulizalisha tani 99,000 zenye thamani ya Sh bilioni 176.3 sawa na asilimia 53.0 huku uzalishaji kitaifa ukiwa ni tani 187,000.3 sawa na asilimia 67 ya lengo la kuzalisha tani laki 280,000.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amezisisitiza taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mabenki kuwa zijitahidi kuwaangalia wakulima hao katika muda wote kuanzia utayarishaji wa mashamba yao mpaka wanapopeleka mazao yao sokoni ili kuwarahisishia wakulima mchakato mzima wa kilimo kupitia mazao wanayolima ikiwemo zao hilo la korosho, ufuta na mengine.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariamu Chaurembo amewasisitiza wakulima hao kulima mazao mengine mbadala wa korosho ili kukuza uchumi endelevu lakini pia wana imani kubwa na MAMCU ambapo ajenda yao kubwa ni kuongeza uzalishaji kama walivyojipangia.

‘’Sisi tuna imani kubwa na chama kikuu cha ushirika cha MAMCU na ajenda yetu kubwa ni kuongeza uzalishaji kama tulivyopanga.” Amesema Chaurembo.

Meneja wa MAMCU, Siraji Mtenguka aliwataka washiriki wa mkutano huo kushirki kikamilifu mkutano kwa kujenga hoja zenye maana ili kusaidia kukijenga chama chao hicho ambacho ni kikubwa na chenye hadhi kubwa hivyo wahakikishe wanakidumisha ili kiweze kupiga hatua kutoka kilipofika kwa sasa kwenda mbele zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button