ZAIDI ya wakulima, wafugaji na wavuvi 2000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamefuaika na elimu ya kilimo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). TABD imetoa mafunzo hayo kushirikiana na shirika la kujitolea la kimataifa(VSO) kupitia mradi wa EYEE.
Akizungumza wakati wa utoaji wa mafunzo hayo leo yaliofanyika mkoani Mwanza Ofisa Maendeleo ya Biashara mwandamizi kutoka (TADB) Angelina Nyasambo, alisema Benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wakulima,wavuvi na wafugaji na wamefanya na vijana ambao wako kwenye vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na ufugaji, kilimo pamoja na wachakataji wa vyakula vya mifugo.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kubadilisha Kilimo kuwa ajira ili waweze kujiinua kiuchumi.
“Baadhi ya vijana hawana ufahamu kazi zinazofanywa na benki yetu na wengine wanashindwa kuifikia ndio maana tumeamua tukutane nao ili tuwaelimishe kazi zinazofanywa na taasisi yetu pamoja na kuwapa elimu ya kukuza biashara zao”, amesema.
Amesema kuwa baada ya mafunzo huwa wanafatilia ili kuona kile ambacho wamewafundisha na kuwaelekeza wameweza kukifanyia kazi kwenye biashara na kuleta tija.
Kwa upande wake Ofisa biashara na mikopo TADB Kanda ya ziwa Janneth Urio, amesema Sekta ya Kilimo inakuwa kwa kasi na ni sekta ambayo inafursa nyingi kwa vijana, wanawake na walemavu.
” Tutaendelea kuwezesha vijana na kuwajengea uwezo ni jambo zuri hususani kwenye sekta ya Kilimo ambayo ni uti wa mgongo na inayo fursa kubwa katika kukuza uchumi wa nchi vijana wanaweza kuwekeza kwenye kilimo na kukigeuza kuwa kilimo biashara ambacho kinaweza kumpatia ajira na fedha na wakaboresha maisha yao”, amesema.
Mshiriki wa mafunzo hayo Leila Peter alisema mafunzo hayo yatamsaidia kubadilisha biashara zao za ufugaji kwa kuzifanya kwa weledi mkubwa kutokana na mbinu mbalimbali walizopewa ikiwemo kuanza kutafuta masoko kabla ya kuanzisha ufugaji.
Comments are closed.