Wakulima wafurahia bei ya nyanya kupaa

BEI ya nyanya mashambani katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa, imepaa kutoka Sh 5,000 kwa tenga la kilo 40 Agosti mwaka jana hadi kati ya Sh 45,000 na Sh 50,000 mwaka huu.

Baadhi ya wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Mtitu wilayani Kilolo, wamesema ongezeko la bei hiyo limefuta kilio cha bei ndogo walichokipata mwaka jana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtitu, Elvis Raban alisema kupanda kwa bei hiyo kumechangiwa na uzalishaji mdogo baada ya wakulima waliopata hasara mwaka jana kukata tamaa ya kuendelea na kilimo hicho mwaka huu.

“Mwaka jana tulikuwa tunaingiza sokoni wastani wa tani 14 hadi 20 za nyanya lakini sasa hivi tunaingiza wastani wa tani tatu tu wakati  mahitaji ni yale yale na hiyo imechangia kupanda kwa bei,” alisema.

Raban alisema katika kijiji chao kuna wakulima zaidi ya 100 wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji cha nyanya kupitia maji wanayopata kutoka Mto Mtitu.

Diwani wa Kata ya Mtitu, Ramadhani Ibrahim alisema; “Kupanda kwa bei ya zao hili ni fursa kwa wakulima wetu. Naendelea kuhamasisha wakulima wazalishe kwa wingi, ili wamudu mahitaji ya soko.”

Ibrahim alisema bei inayonekana sasa sokoni ndio thamani halisi ya mkulima, ambayo inatokana na mahitaji ya soko na uwepo wa bidhaa yenyewe.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button