Wakulima waomba ruzuku ya pampu za umwagiliaji
WAKULIMA wadogo wadogo wa Mkoa wa Iringa wameiomba serikali kuingiza mashine ndogondogo za umwagiliaji katika mpango wa ruzuku ya pembejeo ili vifaa hivyo viwawezeshe kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji hatua itakayowaongezea uhakika wa chakula katika kaya kwa mwaka mzima.
Ombi hilo limetolewa na wakulima hao walioshiriki kongamono la wadau wa kilimo cha umwagiliaji lililofanyika mjini Iringa kwa uratibu wa taasisi ya KickStart inayojishughulisha na usambazaji wa pampu za umwagiliaji za MoneyMaker.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa, Paul Mwinuka alisema; “Kuna haja pampu hizo zikaingizwa katika mpango wa ruzuku ya pembejeo kwani zinaweza kuwa mkombozi wa wakulima wadogo kwa kuzingatia ubora wake na unafuu wa gharama zake.’
Alisema pampu za umwagiliaji hupunguza upotevu wa maji, umwagiliaji wa mkono au wa kutegemea mvua, gharama za uzalishaji na huongeza tija na kuruhusu wakulima kujikita katika shughuli nyingine za kilimo na hivyo kuongeza mapato yao.
“Kama serikali inavyofanikiwa kuongeza tija katika kilimo kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, ikifanya hivyo kwa kuwapatia mashine ndogondogo za umwagiliaji, uzalishaji hususani wakati wa kiangazi utaongezeka,” Mwinuka alisema.
Meneja wa Kick Start Kanda ya Afrika Mashariki Pascal Maitha alisema taasisi yao imefanya utafiti na kuja na teknolojia ya pampu hizo rahisi ikiwalenga zaidi wakulima wadogo ambao mchango wao katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo nchini unahitajika kwa kiwango kikubwa.
Maitha alisema pampu zao zinazoendeshwa kwa kukanyagwa kwa miguu zina uwezo wa kusambaza maji katika eneo tambarare na mlima kwa umbali wa mita 150 na 200.
“Hata kwa wakulima wenye mashamba madogo madogo nje ya nyumba zao wanaweza kutumia pampu hizi kuzalisha mazao ya aina tofauti tofauti yakiwemo ya mbogamboga kwa mwaka mzima,” alisema.
Alisema kilimo cha umwagiliaji nchini Tanzania na katika jangwa la Sahara ni muhimu kwasababu maeneo yake mengi ni kame kwasababu hayapati mvua za kutosha.
Akizungumzia jinsi kilimo cha umwagiliaji kinavyoweza pia kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Maitha alisema wakati takwimu zinaonesha Tanzania ina hekta zaidi ya Sh milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji zinazotumika ni chini ya asilimia 4.
“Ingawa Tanzania ina eneo kubwa linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji bado fursa hiyo inayoweza kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 50 haitumiki vizuri na badala yake sehemu kubwa ya wakulima hususani wadogo kilimo chao kimeendelea kutegemea mvua ambazo si za kutabirika,” alisema.
Akifungua kongamano hilo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Elias Luvanda aliipongeza taasisi hiyo kwa kuja na teknolojia hiyo akisema wakulima wanaweza kuitumia kudhibiti upotevu wa maji na kuhakikisha mimea inapata maji ya kutosha.
Alisema kwasababu maji ni rasilimali adimu hususani katika maeneo yenye ukame, ni muhimu kutumia mifumo ya uhifadhi wa maji ya mvua au kutumia mabwawa ya maji kuhifadhi maji kwa matumizi ya umwagiliaji.
“Na ili jambo hili la kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji lifanikiwe ni muhimu wadau mbalimbali wakendelea kushirikiana na serikali kutoa elimu ay mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu bora za kilimo cha umwagiliaji,” alisema.