Wakulima wapatiwa mafunzo matumizi ya mbegu

ZAIDI ya wakulima milioni 30 nchini wa mazao mbalimbai ikiwemo korosho, mahindi na alizeti wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu, mbolea na mbegu katika mashamba yao.

Akizungumza wiki hii katika maonesho ya Nane nane Kanda ya kusini yanayofanyika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, Meneja wa Matawi ya Kampuni ya ETG Inputs Tanzania Limited ambaye pia ni Ofisa kilimo mkuu wa kampuni hiyo Victor Simon, amesema katika kipindi hicho cha maonesho  imekuwa ni fursa kubwa kwao kukutana na wakulima mbalimbali ikiwemo wakubwa, wadogo.

Amesema mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa kwasababu ni zaidi ya miaka mitano mfululizo wamekuwa wakiwahudumia kwenye eneo hilo la Ngongo na matokeo ni makubwa kutokana juhudi zao zimekuwa zikionekana  kwani wamepiga hatua katika kazi yao hiyo hasa suala la kipato na kati ya wakulima hao milioni 30 waliyopatiwa mafunzo, elfu 10,000 ni kutoka Kanda ya Kusini ikiwemo Lindi, Ruvuma na Mtwara.

‘’Lengo ni kuwaongezea kipato kwasababu wengi wanajihusisha na kilimo cha korosho, ufuta, alizeti ambacho ni kilimo cha msimu lakini tumekuwa tukiwapatia mafunzo haya ili waweze kulima na mbogamboga kwasababu ardhi ya huku inauruhusu pia uzalishaji wa mazao ya mbogamboga kwahiyo tunatoa mafunzo ya kitaalam lengo ni kumfikia mkulima moja kwa moja na kumhakikishia mkulima kwamba anavitumia kwa usahihi na anapata matokeo chanya.” amesema Simon

Meneja huyo ameeleza zaidi kuwa, matarajio yao ni kuona mkulima ananufaika na bidhaa hizo anazozipata kutoka katika kampuni hiyo ‘’Mkulima anavyoendelea na sisi ndivyo tunavyoendelea na jitihada zetu za kuwahudumia wakulima wetu.” amesema

Kampuni hiyo inajishughulisha na mambo manne ikiwemo uuzaji na usambazaji wa mbolea za kilimo, usambazaji wa viuatilifu vya kilimo, mbegu za mboga mboga na mahindi pamoja utaoji wa mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo.

Ofisa kilimo wa kampuni hiyo, Daudi Panja amezitaja baadhi ya mbolea wanazosambaza na kutoa huduma kwa wakulima hao ikiwemo za kupandia, kukuzia mazao mbalimbali, kuzalishia, kupulizia na zingine.

Habari Zifananazo

Back to top button