WAKULIMA nchini wameshauriwa kukata Bima ya mazao ili iwakinge na maafa mbalimbali na kuwapa uhakika na usalama wa shughuli zao kabla na baada ya kupata maafa yatokanayo na changamoto za kilimo.
Afisa Bima wa NIC Insurance Experius Nchanila akiongea na HabariLeo katika Maonyesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba’ katika Banda la NIC amesema NIC imeanzisha bima hiyo ya kilimo kwa vile kilimo ni fursa ya ajira, kilimo ni chakula, inatoa mali ghafi katika viwanda na inachangia asilimia 28 ya pato la taifa.
“Kilimo ni uti wa mgongo, asilimia kubwa ya watanzania wanategemea kilimo.”Amesema Nchanila na kuongeza
“Hata hivyo, Kilimo kimezungukwa na changamoto nyingi ikiwa za majanga yasiyoepukika, mfano mafuriko, moto, ukame, wadudu, wanyama wasiodhibitika, hivi vyote uathiri zaidi kilimo.”Amesema
|Amesema, kupitia changamoto hizo, wakulima wengi wamekuwa wakipata tabu na kupoteza mitaji yao, wanashindwa kupata kilimo chenye tija.
“Sasa NIC insurance imekuja na suluhisho la majibu kwa kuwaletea bima ya kilimo, inakinga majanga yote, inamuhakikishia mkulima anapowekeza pesa yake na nguvu kazi aliyoweka kwenye kilimo haiwezi kupoteza.”Amesema
Aidha, amesema vigezo vya kukata bima hivyo ni kuwa na vielelezo ambavyo vinaonyesha umiliki halali wa shamba, awe anazingatia taratibu za kilimo, historia ya eneo hilo au shamba alilokatia bima, historia ya hali ya hewa ya eneo hilo na aeleze ni zao gani ambalo analikatia bima.