Wakurugenzi watano kikaangoni, wapewa siku 90

DODOMA: WAKURUGENZI watano wamepewa siku 90 kuhakikisha wametenga fedha za utekelezaji wa afua za lishe kulingana na idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Agizo hilo limetolewa leo Agosti 29, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki wakati akifungua  mkutano wa mwaka wa tathimini ya saba ya utekelezaji wa mkataba wa lishe nchini.

Wakurugenzi hao ni wa kutoka Halmashauri za Mpanda DC, Kasulu DC, Mkalama DC, Uyui DC na Lushoto DC.

Advertisement

“Kuanzia sasa naelekeza kwa Halmashauri yoyote ambayo itakuwa haijatoa pesa zote, bakaa itakuwa deni la Halmashauri husika na itabidi iongezwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata.”Amesema Kairuki na kuongeza

“Hii ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, Mamlaka za Serikali za Mitaa tuwe tumefikia kiasi cha sh bilioni 67 ambazo tunatakiwa kuchangia kutekeleza Mpango Jumuishi wa Pili wa Lishe wa Taifa ambayo ni asilimia 10 ya bajeti yote ya lishe nchini kwa kipindi cha miaka mitano.” Amesema Kairuki

Kairuki ametoa  rai kwa wakuu wa Mikoa kusimamia Halmashauri zao kwa kuhakikisha fedha iliyopangwa kutekeleza afua za lishe zinatolewa kwa wakati.

“Hii inatokana na matokeo niliyo nayo ambayo inaonekana kuwa kiashiria hiki bado hakitekelezwi ipasavyo katika maeneo mengi. Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe kuwa fedha zinazotolewa zinaenda kutekeleza shughuli zilizopangwa na sio vinginevyo.” amesisitiza Kairuki

Amesema Ofisi ya Rais -TAMISEMI itaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji ili kuwabaini wanaofanya udanganyifu katika matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe na kuchukuwa hatua stahiki.

Aidha, amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa afua za lishe ikiwemo kufanya kaguzi za mara kwa mara za matumizi ya fedha za lishe ili kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa huduma mbalimbali.

8 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *