Wakuu wa magereza hatarini kung’olewa

KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza, Ramadhani Nyamka amesema wakuu wa magereza nchini watapimwa kwa utendaji kazi wao na wasiotosha wataondolewa. Nyamka alisema hayo Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka 2022/23 wa wakuu wa magereza na maofisa waandamizi wa jeshi hilo.

Alisema amekua akitoa maelekezo mengi kwa barua na njia ya simu lakini hilo pekee halitoshi ndio maana wameandaa mkutano kupeana maelekezo.

Nyamka alisema baada ya kikao hicho cha siku mbili watajua nani atoke na nani abaki kwa sababu tayari watakuwa wamepeana maelekezo ya kutosha ya kiutendaji.

Advertisement

“Tunataka kuona kuna weledi katika utendaji kazi, tutawapima wakuu wa magereza nchini kwa utendaji kazi, kwa sababu wananchi wanataka kuona matokeo chanya ya Jeshi la Magereza,” alisema.

Nyamka alisema atakayekiuka maagizo ya sasa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa sababu tayari atakuwa ameshapata maelekezo.

“Mambo yakiwa mabaya wa kunyoshewa kidole ni mimi na hilo sitalikubali na kama mtu asipotimiza wajibu wake lazima aondolewe,” alisema. Alisema wanataka kubaini changamoto, mafanikio na namna ya kujipanga ili kutekeleza majukumu ya kila siku kwa urahisi.

Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu alisema miongoni mwa ajenda ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili ni namna ya utunzaji siri na Nyaraka za Jeshi la Magereza. Aliwataka wakuu wa Magereza pamoja na maofisa waandamizi wa jeshi hilo kuhakikisha wanazingatia mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo ili kuweza kujifunza na hatimaye kuboresha utendaji kazi wao.