Walemavu wa miguu sasa kuendesha magari wenyewe

MTAFITI na mbunifu wa kifaa maalum kinachomwezesha mtu mwenye ulemavu wa miguu kuendesha gari, Joseph Taifa  amesema ni muda sasa watu hao kujitokeza kwa wingi kusomea fani ya udereva kutokana na suluhu ya changamoto yao kupatikana.

Akizungumza jijini Dar es Salaam , Taifa amesema  alifanikiwa kutengeneza kifaa hicho kwa msaada wa fedha kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) baada ya kujiridhisha na ubunifu wake ambao utasaidia jamii katika kutatua changamoto za watu wenye ulemavu wa miguu.

Katika kipindi cha mwaka 2018  mpaka 2022, COSTECH  imefanikiwa kuwatambua wabunifu 2,647 waliofanya kazi nzuri za ubunifu na kuleta suluhu za changamoto katika jamii.

Advertisement

pharmacy

Aidha katika kipindi hicho kiasi cha Sh Bilioni 4.26 zimetumika kwa wabunifu 178 kuwezeshwa, ili waweze kuendeleza vitu walivyobuni kwa manufaa ya wananchi.

Taifa amesema yeye aliamua kubuni kifaa hicho baada ya kumaliza chuo na kuona changamoto zinazowakuta watu wenye ulamavu wa miguu kuendsha magari,  hivyo aliona ni vema kufanya utafiti na jinsi gani kundi hilo litaweza kuendesha gari kama walivyo watu wasio na ulemavu wa miguu.

“Ukishapoteza miguu basi kuendesha gari ni shida na wengi wa walemavu walishakata tamaa ya kuendesha gari, lakini kifaa hiki kinafungwa bila kuharibu gari, lakini pia kinaweza kutolewa pia na gari kubaki katika hali yake ya awali.

Taifa amesema kifaa hicho kimefanyiwa majaribio mengi na hata Shirika la Viwango nchini (TBS) imekithibitisha kuwa ni salama, hivyo wote wanaohitaji kufungiwa ni lazima kwanza wafundishwe kwa kwenda shule ya udereva kama walivyo madereva wengine.

“Wakati tunaendelea kutengeneza vifaa hivi, lakini pia tunaendelea na maandalizi ya shule ya udereva kwa kufuata vigezo vya serikali, ili mtu anapofungiwa basi ajue jinsi ya kutumia lakini vinginevyo wanaweza kusababisha ajali nyingi barabarani kwa kuwa hawana elimu ya kutumia mfumo huo kuendesha gari,”amesema  Taifa.

Taifa ameeleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kutengeneza vifaa 22 na kati ya hivyo wamefunga magari mawili pekee, ambapo gharama za kufunga kifaa hicho ni Sh 600,000 kwa gari moja

“Hizi taasisi za Serikali zinasaidia sana kutuibua maana unaweza kuwa na ubunifu mzuri, lakini huna fedha za kuendeleza, hivyo mimi naishukuru Serikali kupitia COSTECH kuniwezesha hadi kutengeneza kifaa hiki na kuwa na darasa maalumu la walemavu ili waweze kuvitumia,” amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *