Walengwa Tasaf watakiwa kutimiza masharti

WALENGWA wa mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya nne, wametakiwa kutimiza masharti ya msingi ya ruzuku ya fedha wanazopokea ili kuimarisha sifa za kuwa kwenye mpango.

Akizungumza wakati wa ugawaji ruzuku ya fedha, Mratibu wa Tasaf Halmashauri ya Arusha, Grace Makema, alisema fedha hizo zinatolewa kwa walengwa zikiwa na masharti.

Masharti hayo ambayo walengwa wametakiwa kuzingatia masharti ni pamoja na afya kwa kaya zenye watoto wa kuanzia miaka sifuri hadi mitano kwa kuhakikisha wanahudhuria kliniki kwa kipindi chote pamoja na kupata chanjo zote stahiki.

Pia kaya zenye watoto wa miaka sita hadi 18, zinatakiwa kuhakikisha wanakwenda shule na kuhudhuria masomo kwa siku zote bila kukosa huku wakiwapatia watoto hao mahitaji muhimu ya shule.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Laroi, Remingi Joseph, alisema uwapo wa programu mbalimbali za mafunzo kwa walengwa unawasaidia kupata uelewa wa pamoja juu ya miradi ya Tasaf na ruzuku za fedha wanazopokea walengwa.

Awali katika dirisha la mwezi Julai/ Agosti, jumla ya Sh milioni 617.1, zimetolewa kwa kaya 12,288 katika vijiji 88 vya Halmashauri ya Arusha. Kaya zilipokea fedha kwa njia ya simu, benki na fedha taslimu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button