Walimu, mume, mke, watoto wakutwa wamekufa

Walimu, mume, mke, watoto wakutwa wamekufa

MIILI ya wanafamilia wanne wa familia ya walimu akiwemo baba, mama na watoto wawili imekutwa ndani ya nyumba yao ikiwa imeanza kuharibika.

Wanafamilia hao walikuwa wakiishi katika Kitongoji cha Kibumbe, Kata ya Kiwira wilayani Rungwe eneo ambalo siku moja iliyopita gazeti hili liliripoti taarifa kuhusu mwanamke Tabu Masegela kutuhumiwa kumuua na kumzika mumewe, Aron Mwanjisi kutokana na ugomvi wa kimahusiano.

Mdogo wa marehemu wa kike, George Jehak alidai kuwa dada yake aliyemtaja kwa jina la Fortunatha George alikuwa anafundisha katika Shule ya Msingi Ikuti wilayani Rungwe.

Advertisement

Jehak alisema mume wa dada yake hakumtaja jina alikuwa akifundisha katika shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Mbuja.

Alidai kuwa dada yake alikuwa amekwenda huko likizo nyumbani kwake na kwamba walianza kupata mashaka baada ya kutokuwepo mawasiliano kwa muda mrefu na familia ya dada yake.

Jehak alisema walipofika hapo walikuta milango imefungwa na kulikuwa na harufu kali ikitoka ndani ya nyumba na kwenye banda la mifugo kulikuwa na nguruwe aliyekufa.

“Tulipoingia humo ndiyo tulikuta mapanga chini na nyundo na mezani tukakuta sumu…yaani hizi dawa za kumwagilia mboga na kikombe na kijiko pale mezani,” alisema.

Alidai kuwa dada yake na mumewe hawakuwa na maelewano na kulikuwa na mgogoro wa kifamilia.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk Vincent Amei alisema waliokufa kwenye tukio hilo ni baba, mama na watoto wa kike na kiume.