Walimu wa uhandisi kupelekwa viwandani kujifunza

WALIMU wanaoanza kazi katika vyuo vya uhandisi wameandaliwa programu mahususi ya kwenda kujifunza viwandani na kupata ujuzi ikiwa ni moja ya kuifanya elimu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mratibu wa programu ya kukuza ushirikiano kati ya vyuo vya uhandisi na viwanda kusini mwa Jangwa la Sahara (HEPSSA), Profesa Bravo Nyichomba akizungumza katika warsha iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kuwa kupitia programu hiyo, walimu hao vijana watashirikiana na wanafunzi waliopelekwa viwandani ili kutatua changamoto zitakazokuwa zinajitokeza.

“Tumekuwa na ushirikiano na viwanda kwa kupeleka wanafunzi wakapate ujuzi viwandani. Lakini katika programu hii, tunataka tupelekeke walimu hasa wa uhandisi hasa wale vijana wanaoanza kazi ili wakajifunze kazi za mikono na kupata ujuzi,” amesema mratibu huyo.
Alisema kuwa kabla ya programu hiyo inayofadhiliwa na Uhandisi cha Royal Academy cha Uingereza,” wasomi wa vyuo vikuu wanaofundisha masomo ya uhandisi walikuwa walikuwa wakija na utafiti na ubunifu wa kutatua matatizo ya viwanda baada ya kutafakari wenyewe ilhali wenye viwanda wakiwa hawana habari.
“Lakini kama tutakuwa tunafanya kazi toka mwanzoni pamoja na wao, wote tunashirikiana na si ajabu wao wanaongoza njia, tafiti zetu zitachukuliwa… kuliko wewe unaamua tu unawapelekea, wewe ni nani? Una akili sana kuliko wao?” msomi huyo alihoji.
Kupitia utaratibu huo kupeleka walimu na wanafunzi kujifunza viwandani, Prof Nyichomba aliongeza, matokeo yake yatakwenda kutatua tatizo la kitaifa.

Akifungua warsha hiyo iliyohudhuriwa na washiriki kutoka vyuo mbalimbali nchini ambavyo vinatoa elimu ya uhandisi, Naibu Makamu Mkuu (Utafiti) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof Nelson Boniface alisema kupitia programu hiyo, wanataaluma wasiopungua 21 watapelekwa viwandani kujifunza kwa vitendo.
Alisema watakaopelekwa huko watajifunza kwa siku 30 katika utaratubu utakaoanza Septemba 30, 2023 hadi Septemba, 2024.
“Utakuwepo udhamini kwa angalau wahadhiri watatu kutoka makampuni ya ndani, kuandaa warsha tatu kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu na viwanda vya ndani chini ya udhamini wa chuo cha Uhandisi cha Royal Academy kilichopo Uingereza,” Naibu huyo alisema.
Naye Melina San Martin kutoka Royal Academy alisema programu hiyo itasaidia kuondoa pengo kati ya masomo ya darasani na viwanda na kuyafanya yawe kwa vitendo zaidi.

Washiriki katika warsha hiyo walitoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MUST) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB).

Habari Zifananazo

Back to top button