Walimu wakuu waagizwa kuwalinda mabinti

WALIMU wakuu wa shule za Pemba wametakiwa kusimamia mwenendo wa wanafunzi kuhakikisha kwamba wanapambana na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia ambayo ni kikwazo katika maendeleo ya elimu.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alipokutana na walimu wakuu wa shule za Wete, Pemba.

Alisema miongoni mwa changamoto kubwa na vikwazo kwa mtoto wa kike kuendelea na masomo yake ni kuwepo kwa udhalilishaji wa kijinsia.

“Nawataka walimu wakuu kuhakikisha hakuna matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto wa kike yanayotishia mustakabali wa maendeleo ya elimu ya juu ikiwemo mimba,” alisema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,  Mwanaisha Ameir aliwataka walimu kukumbuka maadili ya kazi yao na kujiepusha na matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanafunzi.

Alisema wizara haitasita kumfukuza kazi mwalimu atakayebainika kumpa ujauzito mwanafunzi wa shule.

“Walimu wote mara wanapoajiriwa wanatakiwa kuyatambua majukumu yao ambayo ni kuepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanafunzi ikiwemo mimba,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Piki Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Haji alisema wamefanikiwa kufikisha elimu ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa walimu na wanafunzi ambapo hakuna matukio ya wanafunzi kupata ujauzito na kusababisha kuacha masomo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button