Walimu waliocheka mtoto akichapwa wasimamishwa

KATIBU Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila amewasimamisha kazi watumishi watano akiwamo Mratibu Elimu Kata ya Kakanja na walimu wanne waliokuwa wanacheka wakati mwalimu Isaya Emmanuel ikiwaadhibu watoto kwa fimbo.

Nguvila ameamua hivyo kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila aliyeagiza watumishi hao wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.

Waliosimamishwa kazi ni Mratibu Elimu Kata ya Kakanja, Sweatbert Kiiza na walimu
Godson Rwabisho, Beatrice Kaburanyange, James Josiah na Delphina Leonce.

Pia walimu watatu kati ya hao wamehamishwa kituo cha kazi na wamepewa barua ya onyo.

Mmoja wa wazazi wa watoto waliopewa adhabu ya viboko ambaye pia ni mwalimu wa shule ya Kakanja, Modesta Richard alisema mwanawe anaendelea vizuri na anaendelea na masomo.

Emmanuel alikuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, ameshushwa cheo, amesimamishwa kazi na anaendelea kuchunguzwa kuhusu tukio hilo la Januari 10 mwaka huu.

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kyerwa, Yohana Marwa aliomba radhi kwa kitendo cha mwalimu huyo kutoa adhabu kwa wanafunzi hao.

Marwa alisema wametoa taarifa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) kuhusu tuhuma dhidi ya mwalimu huyo.

Chalamila alisema mwalimu Emmanuel alitumia mamlaka yake ya Mwalimu Mkuu kuchapa viboko wanafunzi zaidi ya mmoja na kuna walimu waliokuwa pembeni wakishuhudia huku wakicheka.

Aliwataja wanafunzi waliochapwa ni Salmon Kakwezi (9) anayesoma darasa la nne na Anord Kweyamba (10) anayesoma darasa la nne.

Habari Zifananazo

Back to top button