Walimu wanaozunguka hifadhi wapewa mafunzo
UONGOZI wa hifadhi za Taifa za Ibanda, Kyerwa na Rumanyika, Karagwe umetoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya maarifa ya jamii ngazi ya shule za msingi na Geographia kwa ngazi ya sekondari.
Pia wametoa mafunzo kwa waratibu wa elimu kata, maofisa elimu juu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira kwa shule zote zinazozunguka hifadhi hizo.
Kamishina msaidizi wa uhifadhi kutoka hifadhi hizo, Frederick Mofulu alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kujenga uelewa kwa walimu wa masomo hayo juu ya masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira na walimu hao watayatumia masomo hayo kuwafundisha wanafunzi shuleni na kutoa elimu katika vijiji wanavyoishi.
Alisema tangu uongozi wa hifadhi hizo uanze kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira mwaka 2021, tayari vijiji 23 vimepata mafunzo jambo ambalo limeimairisha ushirikiano mzuri na urafiki kati ya uongozi wa hifadhi na wanakijiji tofauti na hapo mwanzo.
“Lengo la mafunzo ni kujenga kizazi salama ambacho kitajua maana ya uhifadhi, tunataka baadae watoto wadogo wawe mabalozi wazuri wa kupinga masuala ya ujangiri.
“Mwanzoni wakati hifadhi zetu zinafunguliwa kulikuwa na matukio makubwa sana ya ujangili na uwindaji haramu wa wanyama, lakini tangu tuanze kutoa mafunzo kumekuwepo na uelewa mkubwa wa wananchi wanaotoa taarifa mapema kabla ya tukio baya kutokea ndani ya hifadhi zetu, “alisema Mofulu.
Alisema viongozi wa vijiji wameendelea kuwa sehemu ya ulinzi wa hifadhi hizo, jambo ambalo limeendelea kuongeza wanyama na kuvutia watalii katika hifadhi za Ibanda, Kyerwa na Rumanyika Karagwe.
Katibu tawala Wilaya ya Karagwe Benjamin Mwakasege anakiri mabadiliko makubwa yaliyopo tangu kuanzishwa kwa hifadhi hizo, ikiwemo uwepo wa mvua za kutosha, baadhi ya vyanzo vya maji kupunguza kukauka pamoja na Vijiji ambavyo havikuwa na miundombinu kuwa na barabara, ili kuwezesha wageni kufika hifadhini kwa urahisi.
Aliwataka walimu na waratibu wa elimu kuhakikisha masomo ya uhifadhi wanayafanyia kazi kwa kuwafundisha wanafunzi vizuri, kwani njia hiyo inaweza kuwa sehemu ya ajira kwao kwa miaka ya baadae, kama watajikita kujifunza vizuri uhifadhi, lakini kuwa sehemu ya kuwafundisha wanakijiji waliozunguka hifadhi hizo masuala ya faida za uhifadhi katika jamii wanayoishi.