Walimu wapendekeza elimu ya lazima miaka 11

WALIMU wa shule za sekondari, wakufunzi na wahadhiri wa vyuo mbalimbali, wameshauri elimu ya lazima iwe ya miaka 11 badala ya miaka 10 kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya sera na mitaala ya elimu.

Aidha, walimu hao wameshauri kuwa falsafa ya elimu iendelee kuwa elimu ya kujitegemea kwani wanadhani bado inatosha kuendelea kuwa falsafa ya elimu ya Tanzania na pia lugha ya kufundishia iwe kiingereza kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu na pia lugha ya Kihispania na Kireno ziongezwe.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake kwenye kongamano la sera na mitaala ya elimu mjini Dodoma jana, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Muhange Kakonko mkoani Kigoma, Zamoyoni Uzale alisema kwa maoni yao wanaona hayo yakifanyika yataboresha elimu.

“Pia fani zote katika mkondo wa elimu ya amali zifundishwe katika shule zote ili wanafunzi wachague kulingana na mahitaji… tunadhani kufunga baadhi ya shule kufundisha fani fulani itasababisha wanafunzi wengine kukosa fursa ya kuchagua kulingana na mahitaji yao,” alisema Uzale ambaye ni mwalimu wa somo la Historia.

Kuhusu elimu kuwa ya miaka 11 badala ya 10 kama mapendekezo yanavyosema, Uzale alisema sera imeuacha mwaka mmoja wa awali hivyo wanapendekeza umuhimu wa elimu ya awali na hivyo sera itaje elimu lazima iwe ya miaka 11.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa serikali na taasisi, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba alisema muundo wa mfumo wa elimu haujazingatia wanafunzi wenye mahitaji maalumu hasa viziwi, ulemavu wa akili na usonji kwani wanahitaji muda zaidi wa kusoma.

“Kamati imesita kidogo baada ya kuona sera inazungumzia elimu ya amali hasa kufundishwa kulingana na maeneo ya kijiografia, inatoa angalizo kwamba tunaweza kuwa na elimu ya kikandakanda ya kimaeneo inaweza kupunguza ule muingiliano ambao tumeurithi toka uhuru, tamko husika 3.3 11 liboreshwe,” alisema profesa Ndomba.

Aidha alisema pia tamko la 3.3.29 liboreshwe kwa kuongeza lugha ya alama ili kurahisisha mawasiliano shuleni kwa wanafunzi wenye uziwi, kutoona.

“Umri wa kuanza shule kwa watoto wenye mahitaji maalumu haujawekwa, kwenye sera iainishwe vizuri maana wale wanaweza kuanza wamechelewa miaka saba, minane kutokana na uchelewaji wa utambuzi,” alisema profesa Ndomba.

Mwenyekiti wa Kongamano Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda alisema watazingatia maoni yaliyotolewa kwenye kongamano hilo.

Profesa Mkenda alisema kuhusu suala la tehama, kampuni ya simu ya Airtel wamempa mapendekezo ambayo atayafanyia kazi na kuzitaka kampuni nyingine kujitokeza wafanye kazi.

Naibu Waziri ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Deogratius Ndejembi aliwahakikishia wadau wa elimu kuwa wizara hiyo iko tayari kufanya maboresho na kuifanya elimu ya Tanzania kuwa bora.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alisema alikuwa na lengo la kupata maoni kwenye rasimu ya sera na rasimu ya mitaala na maoni mengi yametolewa.

“Kupitia majadala huu tumeona maeneo mazuri ya kufanyia kazi na michango yenu itakwenda kuchakatwa tena,” alisema profesa Nombo.

Mwakilishi wa wadau wa maendeleo kutoka Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), DeoKapichi alisema kuwa mapitio hayo yanakwenda sambamba na mipango ya kimataifa ya mapitio ya elimu.

Makamu mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Rose Mariki alisema Rais Samia Suluhu Hassan alikuja na wazo zuri la kuangalia mahali pa kuboresha.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Mali Zanzibar, Mtumwa Idd Hamad alisema waashirikiana kuhakikisha azma ya serikali inatekelezwa kwa vitendo.

Imeandikwa na Zena Chande (Dar es Salaam) na Sifa Lubasi (Dodoma).

Habari Zifananazo

Back to top button