CHAMA cha Walimu wa Hisabati nchini (CHAHITA), kimeiomba serikali kulipa kipaumbele somo la hisabati, kwani kwa sasa hali ya ufaulu ni hafifu kwa ngazi zote za elimu hasa kwa shule za msingi na sekondari.
Somo hilo kwa kipindi cha miaka tisa iliyopita, ufaulu kwa shule za msingi ni asilimia 31.86 na sekondari ni asilimia 17.46, ambapo kwa mwaka 2021 ufaulu kwa kidato cha nne ulikuwa asilimia 19.54 na kulifanya kuwa la mwisho kwa ufaulu kitaifa.
Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Betinasia Manyama amesema hayo Agosti 31, 2022 mjini Morogoro, kabla ya kumkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, kufungua mafunzo ya kitaifa ya 56 ya Hisabati na Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA alimwakilisha Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ambapo mafunzo na mkutano huo unaofanyika Kampasi ya Solomon Mahlangu mkoani Morogoro.
Manyama ametaja sababu zinazosababisha somo hilo kuwa na ufaulu hafifu ni hamasa ndogo kwa walimu na wanafunzi, upungufu wa walimu kitendo kinachochangia kuwa na vipindi vingi kwa siku, mwezi hadi mwaka ikilinganishwa na masomo mengine.
“Ni vyema serikali kulipa somo la Hisabati umuhimu maalumu, maana ndio nguzo ya masomo yote mengine hasa masomo ya sayansi, bila ya hisabati, ukweli ni kwamba hakuna maisha, bila ya hisabati hakuna wahandisi na hivyo hakuna viwanda,” amesema Manyama.
Manyama ameiomba serikali kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, kuwaongeza malipo ya ziada walimu wa hiasabati na wale wenye ufanisi zaidi wa kufundisha, ili itoa motisha kwa walimu waweze kujituma zaidi.
Pia ameomba somo hilo liingizwe kwenye vigezo vya ufaulu wa daraja la kwanza na pili katika matokeo ya kitaifa ya kidato cha nne, ili kuongeza chachu kwa wanafunzi wengi zaidi kuweza kulipenda na kujifunza somo hilo.
“ Tanzania haiwezi kuwa na uchumi imara na endelevu endapo ufaulu wa somo la hisabati utaendelea kuwa chini, somo hili ni msingi wa maendeleo kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi,” amesema Manyama.
Kwa upande wake Prof. Chibunda amesema somo la hisabati lina umuhimu mkubwa katika jamii, kwani ndio nguzo ya kukuza uchumi wa nchi.
“Haina shaka kuwa hisabati ndio kitendea kazi katika maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, hivyo katika uchumi wa viwanda hisabati ndio ufunguo wake na wengi tumekombolewa na hisabati kutokana na ufanisi wake,” amesema Prof. Chibunda
Amesema wizara inatambua, hisabati ni somo muhimu na lenye changamoto nyingi katika ufundishaji ngazi zote za elimu.
Amewapongeza wanachama wa chama hicho kwa kuendelea kuonesha juhudi za mafunzo ya somo la hisabati, kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi shuleni.
Awali Mkuu wa Idara ya Hisabati wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sylvester Rugeihyamu, aliziomba halmashauri za wilaya nchini kuwawezesha walimu wa hisabati kushiriki katika mafunzo ya kuwaongezea maarifa.