Walimu Z’bar ziarani Mara

Walimu Z’bar ziarani Mara

WALIMU wasiopungua 50 kutoka Zanzibar, wapo mkoani Mara kujifunza na kuunga mkono mpango wa kukuza utalii, uliyozinduliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia filamu ya Royal Tour.

Wakiongozwa na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wa Mkoa wa Mara, Suzan Shesha walipokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee akisema hawakukosea kuchagua Mara kwasababu ni chimbuko la Tanzania.

“Hata kwenye filamu ya Royal Tour, ukiacha Zanzibar maeneo mengi yanatangaza nchi yetu yapo Mara,” alisema Meja Jenerali Mzee.

Advertisement

Alisema watashuhudia mengi ikiwamo alikozaliwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwamba kila wakitaka kuondoa stress wafike Mara kwa kuwa ziara ya utalii haifanyiki mara moja.

Awali ilielezwa na Makamu wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU), Musa Abdi Hamis sababu za ujio huo kuwa ni kujifunza, wakitarajia kuchukua na kuacha mazuri ya kijamii na kitaaluma kwa wenyeji wao.

“Pia tunaimarisha undugu ulioasisiwa na wazee wetu, Nyerere na Karume kwa kujua kwamba udugu hunoga kwa kutiwa urafiki,” alisema Hamis.

Alisema wamekusudia kukuza utalii kwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia, kupitia filamu ya Royal Tour, kwani ameendelea kufanya mazuri kwa wananchi wakiwamo watumishi.

Naye Shesha alipongeza hatua ya ZATU kufanya ziara hiyo na kuahidi kuwa CWT mkoani Mara itaandaa na kufanya ziara ya aina hiyo Zanzibar, ili pamoja na mambo mengine, kuimarisha undugu na urafiki.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *