Walioathirika gari la gesi kupelekwa Muhimbili

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu mwishoni mwa wiki amekwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya gari lililopinduka eneo la Kwamkono wilayani Handeni mkoani Tanga likiwa na gesi.

Baada ya majadiliano na Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Dk Naima Yusuf, Ummy ameshauri majeruhi hao wapewe rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.

“Kutokana na hali zao kutokuwa nzuri ninashauri majeruhi hao wapewe rufaa na kupelekwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi”alisema.

Advertisement

Gari hilo baada ya kupinduka gesi ilisambaa na kusababisha madhara kwa wananchi wakiwemo walioungua.

Akiwa amefuatana pia na Katibu wa Afya Mkoa wa Tanga, Frank Mhilu, Ummy aliwajulia hali na wagonjwa wengine na akawapongeza wauguzi na madaktari kwa kazi wanayoifanya kuwahudumia wananchi.

Alisema wanaangalia uwezekano wa kulifanyia ukarabati jengo la Clief kwenye hospitali hiyo ili liwe na mwonekano mzuri.