Waliobiwa televisheni, ‘laptop’ waitwa Polisi

DAR ES SALAAM; JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, linamshikilia mkazi wa Makumbusho, Essau Francis (27) maarufu Makumba na wenzake wanne kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba vifaa vya kieletroniki.

Vifaa hivyo ni televisheni, redio na kompyuta mpakato na waliobiwa wameitwa Polisi wakiwa na risiti na RB kutambua mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano kituo cha Polisi Kati, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni inayoendelea ya kuzuia uhalifu iliyoanza Machi mwaka huu.

Muliro alisema baada ya kuwakamata watuhumiwa walihojiwa na walifanya upelelezi wa kina na kufanikiwa kukamata televisheni 35 zilizoibiwa katika maeneo ya Mbweni, Madale, Goba, Kigamboni, Mbagala, Kinondoni na maeneo mengine.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba vifaa vya kielektroniki ikiwemo televisheni kwa kuvunja, kukata madirisha na kupitia milangoni katika nyumba ambazo wanaacha funguo milangoni.

Muliro alisema miongoni mwa televisheni hizo zilizokatwa tayari sita zimetambuliwa na kupatiwa wahusika baada ya kufika kituo cha Polisi na kuonesha risiti ya ununuzi yenye namba ya televisheni husika.

Aidha, aliwataka wananchi ambao wameibiwa vifaa vya kielektroniki kufika vituo vya polisi kati, Mbweni na Chang’ombe kutambua mali zao wakiwa na risiti zinazooenesha uhalali wa umiliki na ‘serial’ namba.

Muliro alisema katika muendelezo wa operesheni hiyo Polisi kanda hiyo imemkamata raia wa Kenya mkazi wa Kimara, Javan Ochieng (36) na wenzake watatu kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kujifanya mawakala wa mafunzo ya biashara, shule, vyuo na ajira kwa vijana nje na ndani ya nchi.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia jina la Kampuni ya Profession Exchange Platfom kuwahadaa watu ili kujipatia fedha kwa madai ya kuwatafutia nafasi katika taasisi mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button