Waliofata mkumbo kwenye maandamano waachiwe

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana nchini kuacha tabia ya kufuata mkumbo, akisema kitendo hicho kimewaingiza baadhi yao katika matukio ya uvunjifu wa sheria bila wao kutambua madhara yake.
Akifungua Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Kwanza jijini Dodoma, Rais Samia amesema vijana wengi waliokamatwa kwa makosa yanayohusiana na uhaini hawakuwa na dhamira ya kutenda kosa bali walijikuta wakiingia kwenye vurugu kwa kushawishiwa na mazingira.
Amesema kutokana na hali hiyo, ameielekeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) kuchambua kwa makini kiwango cha makosa ya vijana hao ili kubaini waliokiuka sheria kwa makusudi na wale waliokwenda bila kutambua uzito wa wanachokifanya. “Kuna vijana kwenye zile klipu za maandamano ambao ni wazi walifuata tu mkumbo. Hawakujua wanalolifanya. Vyombo vya ulinzi na usalama vichuje makosa hayo,” alisema. Rais
Samia aliongeza kuwa msamaha anaoanza nao unatokana na misingi ya dini na maadili ya Kitanzania, ili kuijenga jamii inayoelewana na yenye umoja. SOMA: Rais Samia aviita pamoja vyama vya siasa



